Afisa wa ngazi ya juu wa EU: Mfumo wa dunia unasambaratika
(last modified Wed, 16 Apr 2025 07:52:57 GMT )
Apr 16, 2025 07:52 UTC
  • Von der Leyen
    Von der Leyen

Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya amesema kuwa EU inapasa kuwa na mchango athirifu katika kuasisi mfumo mpya wa dunia huku ikiimarisha uwezo wake wa kijeshi na kiuchumi.

Ursula von der Leyen mapema leo ameeleza kuwa: "Mfumo wa dunia unasambaratika na nafasi yake imechukuliwa na machafuko yaliyosababishwa na ushindani wa Marekani na China na tabia ya kupenda makuu ya Putin."

Akizungumza katika mahojiano na gazeti la Kijerumani la "Zeit" Mkuu huyo wa Kamisheni ya Ulaya amesema: Ulaya inapasa kuanzisha mfumo mpya wa dunia na kwamba "Umoja wa Ulaya umetambua kwamba unapasa kuimarisha nafasi yake ya kiuinzi, kiuchumi na kimataifa."

Von der Leyen ameongeza kuwa: Miaka michache iliyopita kutenga euro bilioni 800 kwa ajili ya nguvu za kijeshi ingekuwa jambo lisilofikirika. "Ulaya sasa inafanya kazi kikamilifu na washirika wake duniani ili kuasisi miungano mipya. 

Kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya ameshiria kuvurugika uhusiano wa kuvuka eneo la Atlantiki na kueleza kuwa: Ulaya inapasa kuchukua hatua ili kujitegemea. "Tunajitahidi kupunguza kuitegemea Washington na Beijing lengo likiwa ni kuanzisha minyororo ya ugavi ya uwiano na mseto", amesisitiza Von der Leyen.