Waziri Mkuu mpya wa Greenland amwambia Trump: Greenland haiuzwi
Waziri Mkuu mpya wa Greenland amesisitiza kuwa Greenland haiuzwi. Jens Frederik Nielsen ameeleza haya akimhutubu Rais wa Marekani ambaye ametaka eneo hilo kuunganishwa na Marekani.
Jens Frederik Nielsen ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari akiwa pamoja na Mette Frederiksen, Waziri Mkuu wa Denmark huko Copenhagen, amemhutubu Rais Donald Trump kwamba: "Abadan Greenland si eneo la kuuzwa, natumai kuwa Wamarekani wanatambua hili."
Waziri Mkuu mpya wa Greenland amesisitiza kuwa nchi hiyo inaimarisha uhusiano wake na Denmark kufuatia kauli za dharau za serikali ya Marekani. "Kuna ulazima kwa Greenland na Denmark kukurubiana zaidi katika mazingira ya sasa ya sera za nje."
Katika mahojiano mbalimbali, Rais wa Marekani, Donald Trump aliweka wazi azma yake ya kuitwaa Greenland na kuiunganisha na Marekani na wakati huo huo hakuondoa uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi ili kufanikisha lengo hilo,
Greenland ina eneo la kimkakati la kijiografia na rasilimali nyingi za madini. Kisiwa hicho ndicho njia fupi zaidi kati ya Ulaya na Amerika Kaskazini.