Kampuni ya Uingereza inaipatia Israel injini za ndege zisizo na rubani (Droni)
Shirika moja la habari la Uingereza limefichua kuwa kampuni ya uhandisi ya RCV Engines ya Uingereza inasambaza kwa Israel injini za kizazi kipya zaidi cha ndege zisizo na rubani zinazotumika kufanya mauaji huko Palestina.
Taarifa hiyo ni ushahidi mwingine unaoonyesha namna London inavyoshiriki katika mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Ripoti hiyo imeweka wazi kuwa picha zilizochapishwa na Kampuni ya Masuala ya Anga ya Israel (IAI) zinaonyesha injini ya droni ya APUS 25 ikiwa na nembo ya Kampuni ya Uhandisi ya Uingereza ya RCV Engines. Droni hizo aina ya APUS 25 zimetengenezwa kwa ajili ya matumizi ya muda mrefu na kutumika katika operesheni za mapigano, na zina uwezo wa kubeba silaha na kufanya oparesheni za ujasusi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na huko Gaza.
Kampuni ya Masuala ya Anga ya Israel (IAI) imesema kuwa droni hizo zina uwezo wa kusalia angani kwa muda mrefu zikiwa zimebeba mizigo.
Ufichuzi huo unatoa ushahidi zaidi kwamba vipuri vya ndege zisizo na rubani zinazotengenezwa na Uingereza vinasafirishwa hadi Israel ili ndege hizo zitumike kufanya uhalifu wa kivita huko Gaza.