Euro-Med: Marekani inatenda kazi kama nguvu iliyo juu ya sheria nchini Yemen
(last modified Wed, 30 Apr 2025 06:47:50 GMT )
Apr 30, 2025 06:47 UTC
  • Euro-Med: Marekani inatenda kazi kama nguvu iliyo juu ya sheria nchini Yemen

Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu la Euro-Mediterania limesema kuwa Marekani inafanya kazi kama mamlaka iliyo juu ya sheria za kimataifa nchini Yemen na inakaidi kanuni za uwajibikaji wa kimataifa.

Euro-Mediterania imesema, wakati machafuko yakiendelea katika eneo la Magharibi mwa Asia, Marekani imejikita katika kuzidisha mivutano na operesheni za kijeshi badala ya kujaribu kutatua chanzo cha migogoro hiyo.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu pia limetoa wito kwa taasisi za kimataifa kuunda kamati huru ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani nchini Yemen.

Taasisi hiyo ya Ulaya imeitaka Marekani kujiepusha kabisa na ushirikiano na Israel katika uhalifu wa kivita dhidi ya raia wa Gaza na kuheshimu kanuni za sheria za kimataifa.

Ikiendeleza jinai zake huko Yemen, Marekani imeshambulia eneo la kaskazini mwa nchi hiyo na kuwaua Wayemeni 12. Ripoti zinasema, watoto na wanawake kadhaa ni miongoni mwa waliouawa katika mashambulizi hayo.

Tangu Machi 15 mwaka huu, Marekani imekuwa ikiusaidia utawala katili wa Israel kwa kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya Yemen ambayo yanalenga maeneo ya makazi na vituo vya raia nchini humo.