Trump amfuta kazi Mshauri wa Usalama wa Taifa na naibu wake
(last modified Fri, 02 May 2025 06:53:35 GMT )
May 02, 2025 06:53 UTC
  • Michael Waltz
    Michael Waltz

Ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zinasema Mshauri wa Usalama wa Taifa, Michael Waltz na naibu wake, Alex Wong, wataacha nyadhifa zao kwa agizo la Rais Donald Trump.

Vyanzo vinne vya ndani vimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba Waltz amelazimishwa kung'atuka na kuondoka kwenye wadhifa huo. Fox News pia imeripoti kuwa, maafisa wengine watalazimika kujiuzulu, na kwamba Trump atazungumzia suala hilo karibuni.

Kuhusu kung'atuka Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Jarida la Wall Street Journal limeripoti kwamba kutimuliwa kwa Michael Waltz kunamfanya kuwa afisa mkuu wa kwanza kupoteza kazi wakati wa muhula wa pili wa Trump.

Jarida hilohilo pia limeripoti kwamba Waltz alikabiliana na ugumu kuwasilisha vipaumbele vya usalama wa taifa vya rais wakati wa mahojiano, na kwamba ana misimamo mikali zaidi kuhusu Ukraine na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika muktadha huo huo, CNN imeripoti, ikinukuu vyanzo, kwamba Waltz alipoteza ushawishi wake katika Ikulu ya White House baada ya kashfa ya kuvujishwa mazungumzo ya siri ya mipango ya Washington ya kuishambulia Yemen kwenye mtandao wa kijamii wa Signal.