Kundi la PKK lavunjwa katika juhudi za kufikia amani na Uturuki
(last modified Mon, 12 May 2025 11:11:40 GMT )
May 12, 2025 11:11 UTC
  • Kundi la PKK lavunjwa katika juhudi za kufikia amani na Uturuki

Kundi la wapiganaji wa Kikurdi (PKK) ambalo limekuwa katika mapigano ya silaha na Uturuki kwa zaidi ya miongo minne, limetangaza kuvunjwa kwake na kumalizika kwa mapambano yake ya silaha.

Kundi hilo la 'wafanyakazi wa Kurdistan' (PKK) limetangaza katika taarifa ya mwisho ya mkutano wake wa 12 leo Jumatatu habari ya kumalizika kwa vitendo vyote vinavyonasibishwa na jina lake, ikiwa ni pamoja na mapambano yake ya silaha dhidi ya serikali ya Uturuki.

Baada ya kufanyika kongamano kaskazini mwa Iraq siku ya Ijumaa, PKK ilisema kuwa imefanya maamuzi ya "kihistoria". Shirika la Habari la Firat, chombo cha habari kilicho karibu na kundi hilo, kiliripoti kwamba, taarifa kutoka kwa kiongozi wa PKK, Abdullah Ocalan iliwasilishwa wakati wa kongamano, ikielezea mitazamo na mapendekezo yake.

Ocalan ambaye yuko jela tangu 1999, alihimiza PKK mnamo Februari kusitisha mapambano yake ya silaha ikiwa ni katika juhudi za kutatua mzozo huo, ambao umesababisha vifo vya zaidi ya 40,000 tangu miaka ya 1980.

PKK ambayo inatambuliwa kama kundi la kigaidi na Uturuki na nchi nyingi za Magharibi, ilitangaza kusitisha mapigano muda mfupi baadaye lakini iliweka masharti ya kuvunjwa kwake, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa kisheria wa mazungumzo ya amani.

Mustakabali wa wanamgambo wa PKK bado haujulikani, haswa kuhusiana na uwezekano wa kuhamia nchi zingine. Maelezo kuhusu makubaliano yoyote ambayo PKK inaweza kupokea kama 'malipo' ya kufutwa kwake hayajatolewa kufikia sasa.