Iran: Machafuko nchini Syria ni kwa manufaa ya Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, machafuko na ukosefu wa utulivu nchini Syria ni kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni na kwamba magenge ya kigaidi na yenye misimamo mikali yanatumia vibaya fursa hiyo kwa manufaa yao binafsi.
Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo katika kikao cha dharura cha mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC kilichofanyika mjini Jeddah, Saudi Arabia na kutilia mkazo wajibu wa kushirikiana zaidi na zaidi nchi za Kiislamu hasa katika kutatua changamoto nyingi za Ulimwengu wa Kiislamu yakiwemo matukio ya Asia Magharibi. Vile vile ametaka nchi za Kiislamu zichukue hatua za kivitendo za kupambana na njama za kulifuta taifa la Palestina kwenye ramani ya dunia kupitia kuwalazimisha wakazi wa Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi kuhama makazi yao.
Amegusia pia matukio hatari yanayotokea nchini Syria na wajibu wa watawala wapya kulinda roho za raia akisisitiza kuwa, machafuko katika nchi hiyo ya Kiarabu na Kiislamu ni kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na magenge ya kigaidi yenye misimamo mikali.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema pia kwamba uhusiano wa nchi yake na Uturuki ni wa kipekee na umesimama juu ya msingi wa kulindwa manufaa ya pamoja ya mataifa haya mawili makubwa jirani ya Kiislamu akisisiza kuwa, jukumu la kulinda uhusiano huo ni la pande zote mbili.
Kwa upande wake, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, mbali na kadhia ya Palestina amesema kuwa, uhusiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni muhimu sana na kuna udharura wa kuchukuliwa hatua za kivitendo cha kuimarisha uhusiano huo katika nyuga tofauti.