Wajapani wapinga safari ya waziri wa Israel katika nchi yao
Wananchi wa Japan wamekusanyika na kupinga safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Israel katika nchi yao na kulaani jinai za Tel Aviv dhidi ya wananchi wa Gaza.
Wafuasi wa Palestina walikusanyika mbele ya jengo ambako mkutano ulifanyika na kujaribu kuvuruga mkutano wa waandishi wa habari wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar nchini Japan.
Video iliyoenea katika mitandao, ambayo pia iliakisiwa na vyombo vya habari vya Kizayuni, inaonyesha kuwa siku ya Jumatano waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina walikusanyika nje ya ukumbi wa mkutano, na baadhi yao wanajaribu hata kuingia katika ukumbi huo wakilalamikia uuwepo wa waziri huyo nchini Japan.
Kwa mujibu wa video hiyo, waandamanaji hao wakiwa wamebeba bendera za Palestina wanapinga uwepo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala wa Kizayuni, na mmoja wao alijaribu kuvuka kizuizi cha usalama ambapo alikamatwa na vyombo vya usalama na kuondolewa katika eneo hilo.
Baadhi ya waandamanaji pia wanaonekana wakiwa wameshikilia picha ya waziri huyo Mzayuni huku mikono yake ikiwa imetapakaa damu, huku wakitoa nara ya "mtenda jinai za kivita".
Gideo Saar aliwasili nchini Japan siku ya Jumanne, na hiyo kuwa ziara ya kwanza ya waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni nchini Japan katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.