Pigo jingine kwa Trump; mahakama yaamuru Harvard iandikishe wageni
(last modified Sun, 25 May 2025 06:36:17 GMT )
May 25, 2025 06:36 UTC
  • Pigo jingine kwa Trump; mahakama yaamuru Harvard iandikishe wageni

Jaji wa mahakama moja nchini Marekani amezuia kwa muda amri ya utawala wa Trump ya kufuta kibali cha kuandikishwa wanafunzi wa kigeni katika Chuo Kikuu cha Harvard.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, sambamba na kuendelea mashinikizo ya utawala wa Trump kwa Chuo Kikuu cha Harvard kwa kisingizio cha kupambana na eti chuki dhidi ya Mayahudi, na uamuzi wa Trump wa kufuta kibali ya kudahili na kuandikishwa wanafunzi wa kigeni katika chuo kikuu hicho maarufu duniani, jaji wa mahakama moja ya Marekani amebatilisha kwa muda amri hiyo ya Trump.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa amri hiyo ya mahakama imepunguza kwa muda wasiwasi wa maelfu ya wanafunzi wa kigeni katika Chuo Kikuu cha Havard ambao walikuwa katika hatari ya kuhamishwa baada ya agizo hilo la utawala wa Trump.

Chuo Kikuu cha Harvard kilifungua kesi katika mahakama ya shirikisho siku ya Ijumaa kupambana na uamuzi wa utawala wa Trump wa kubatilisha idhini ya chuo hicho kudahili wanafunzi wa kigeni. Hatua hiyo ilikuja baada ya Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani kukizuia chuo cha Harvard kuendelea na mpango wake wa kuandikisha wanafunzi wa kigeni.

Utawala wa Trump ulikipa Chuo Kikuu cha Harvard muda wa saa 72 kutoa taarifa kamili kuhusu shughuli za wanafunzi wa kigeni hasa wale walioshiriki kwenye maandamano ya kupinga jinai za Israel huko Ghaza, vinginevyo, kibali cha usajili wa wanafunzi wa kigeni kitabatilishwa kabisa. Lakini Chuo Kikuu cha Havard kimeshinda kesi mahakamani na jaji amebatilisha kwa muda uamuzi wa utawala wa Trump.