Australia: Palestina itatoweka kama mauaji ya kimbari ya Israel yataendelea
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129172
Penny Wong, Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia amesema kuwa kuna hatari kwamba hakutakuwa na Palestina inayoweza kutambuliwa iwapo mauaji ya kimbari ya Israel yataendelea katika Ukanda wa Gaza sambamba na kuongezeka vitendo vya mabavu dhidi ya Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2025-08-05T17:10:13+00:00 )
Aug 05, 2025 14:12 UTC
  • Penny Wong
    Penny Wong

Penny Wong, Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia amesema kuwa kuna hatari kwamba hakutakuwa na Palestina inayoweza kutambuliwa iwapo mauaji ya kimbari ya Israel yataendelea katika Ukanda wa Gaza sambamba na kuongezeka vitendo vya mabavu dhidi ya Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Wong amesema haya leo asubuhi katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Australia (ABC). Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia ameeleza haya akijibu maswali aliyoulizwa kuhusu maandamano makubwa yaliyofanyika Sydney yaliyohudhuriwa na mamia ya maelfu ya watu  kupinga mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza. 

Wasimamizi wa maandamano hayo wameripoti kuwa, kati ya waandamanaji laki mbili hadi laki tatu waliandamana juzi Jumapili katika Daraja la Bandari ya Sydney nchini Australia; idadi inayotajwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Australia. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia amesema kuwa serikali ya nchi hiyo inaunga mkono takwa la waandamanaji nchini la kupatikana amani na usitishaji vita huko Gaza.

Amesema idadi kubwa ya watu waliojitokeza katika maandamano ya Sidney inaakisi wasiwasi na mshtuko ulioipata jamii ya Waustralia kuhusu kile kinachojiri huko Gaza, hali mbaya ya binadamu katika eneo hilo, kuuawa wanawake na watoto na kuzuiwa misaada ya kibindamu kuingia katika eneo hilo. 

Gaza

Takriban Wapalestina 200, wakiwemo watoto 93 wameaga dunia kwa njaa katika Ukanda wa Gaza tangu utawala wa Israel uanzishe vita na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa eneo, Oktoba 7 mwaka 2023.