Uruguay yafunga ofisi yake Quds kuonyesha mshikamano na Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129646-uruguay_yafunga_ofisi_yake_quds_kuonyesha_mshikamano_na_gaza
Serikali ya Uruguay imeamua kusitisha makubaliano ya ushirikiano yaliyotiwa saini mwezi Disemba mwaka jana 2024 kati ya Wakala wa Kitaifa wa Utafiti na Ubunifu wa Uruguay na chuo kikuu cha Israel huko Quds (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu, sanjari na kufunga Ofisi yake ya Ubunifu mjini Jerusalem ili kuonyesha mshikamano na Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-09-23T11:30:28+00:00 )
Aug 18, 2025 02:54 UTC
  • Uruguay yafunga ofisi yake Quds kuonyesha mshikamano na Gaza

Serikali ya Uruguay imeamua kusitisha makubaliano ya ushirikiano yaliyotiwa saini mwezi Disemba mwaka jana 2024 kati ya Wakala wa Kitaifa wa Utafiti na Ubunifu wa Uruguay na chuo kikuu cha Israel huko Quds (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu, sanjari na kufunga Ofisi yake ya Ubunifu mjini Jerusalem ili kuonyesha mshikamano na Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina la Ma’an, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uruguay, Mario Lubetkin ametaja matukio ya hivi karibuni katika eneo la Asia Magharibi na hatua za jeshi la Israel huko Gaza kuwa sababu za uamuzi huo.

Baraza la Mawaziri la Uruguay limeshutumu kitendo cha Israel kuukalia mji wa Gaza na kukitaja kama ukiukaji wa sheria za kimataifa. Ukitoa radimali yake kwa uamuzi huo, Ubalozi wa Israel huko Montevideo umeonyesha masikitiko, ukihusisha uamuzi huo na hitilafu za kisiasa.

Hatua za Uruguay zinafuatia uamuzi wa Israel wa kutwaa udhibiti kamili wa Gaza, kampeni ambayo baadhi ya ripoti zinasema inalenga raia.

Jumanne iliyopita, takriban nchi 24 za Magharibi zilitoa wito wa kuingizwa bila vikwazo misaada ya kibinadamu huko Gaza, huku baadhi yazo, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Uhispania, Australia, Ufaransa, Canada, Luxemburg, Ureno na Ireland, zikitangaza mipango ya kuitambua Palestina katika mkutano ujao wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York.

Ikumbukwe kuwa, Juni mwaka huu, makundi mengi ya kijamii na kisiasa kama Chama cha Kikomunisti (PCU), Harakati ya Artigesta (VA), Chama cha Kisoshalisti (PS) na PVP, yaliitaka serikali ya Rais wa Uruguay, Yamandu Orsi kuchukua msimamo mkali na mgumu zaidi dhidi ya uvamizi, ukiukaji wa haki za binadamu na mauaji ya halaiki huko Gaza.