Kwa nini majimbo ya Marekani yanaadhibiwa kwa sababu ya kuitetea Palestina?
Rais wa Marekani, Donald Trump, ametishia kukata bajeti ya dharura ya kukabiliana na majanga ya asili na kudhamini usalama wa ndani wa majimbo na miji ya Marekani inayounga mkono Palestina na kususia makampuni ya Israel.
Serikali ya Shirikisho ya Marekani, imesisitiza kuwa majimbo na miji inayosusia makampuni ya Israel hayatapewa bajeti za kujitayarisha kwa ajili ya kukabiliana na maafa ya kimaumbile, na kutangaza kuwa: Kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Shirika la Usimamizi wa Majanga la Shirikisho, ili kupokea ufadhili huu, majimbo yanalazimika kuthibitisha kwamba hayatakata uhusiano wao wa kibiashara na makampuni ya Israel.
Uamuzi huu wenye utata, ambao klivitendo umegeuza misaada muhimu ya Serikali ya Shirikisho kuwa chombo cha mashinikizo ya kisiasa dhidi ya wapinzani wa Israel, ni kielelezo kinachotia wasiwasi wa kuongezeka ushawishi wa lobi za Kizayuni katika muundo wa ndani wa Marekani.
Katika miaka ya hivi karibuni, sera za ndani za Marekani zimefungamana zaidi na matukio ya Asia Magharibi, haswa na uhusiano wa nchi hiyo na Israel. Utegemezi na mfungamano huu hauonekani tu katika nyanja za kidiplomasia na kijeshi, lakini sasa umepenya na kuingia katika maeneo nyeti ya ndani kama vile ugavi wa bajeti ya shirikisho. Mfano wazi wa suala hili ni uamuzi mpya wa serikali ya Trump na tishio la kukata bajeti ya dharura kwa majimbo na miji inayounga mkono Palestina au kukata ushirikiano na kampuni za Israel.

Katika miezi ya hivi karibuni, suala la kufukuzwa wanafunzi katika vyuo vikuu mashuhuri vya Marekani kutokana na uungaji mkono wao na kuitetea Palestina au kushiriki katika maandamano ya kupinga vita vya Israel huko Gaza limeakisiwa sana katika vyombo vya habari ndani na nje ya Marekani. Wanafunzi hao wa vyuo viikuu, ambao mara nyingi walikuwa wakiendesha shughuli zao katika harakati za kiraia na za kutetea haki za binadamu, walikabiliwa na aina mbalimbali za hatua za kinidhamu, na katika baadhi ya matukio kufukuzwa vyuoni, kwa sababu tu ya kutoa maoni ambayo hayakuendana na sera rasmi ya Serikali ya Shirikisho ya kuinga mkono Israel. Mienendo kama hiyo ya vyuo vikuu vinavyodai kuwa watetezi wa uhuru wa kujieleza imedhihirisha wazi jinsi uhuru wa kujieleza na harakati za wanaharakati wa masuala ya kiraia unavyobanwa kwa kiwango kiikubwa nchini Marekani, hasa wakati maslahi ya mshirika wa kimkakati wa nchi hiyo, Israel, yanapokuwa hatarini. Uamuzi wa Trump wa kushurutisha bajeti za Shirikisho na suala la kutosusia makampuni ya Israel unapaswa kutathminiwa kama mwendelezo wa mbinu hii. Kwa mujibu wa uamuzi huo, majimbo na miji itakayochagua kukata uhusiano wa kibiashara na makampuni ya Israel kwa sababu za kimaadili, kisiasa au haki za binadamu itanyimwa kwa uchache bajeti ya dola bilioni 1.9 za kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya kimaumbile. Bajeti hiyo kwa kawaida hutumiwa kuandaa timu za utafutaji na uokoaji, kulipa wasimamizi wa migogoro, kuimarisha mifumo ya nishati ya dharura, na kutekeleza majukumu mengine muhimu wakati wa majanga. Kwa ufupi ni kwamba, Serikali ya Federali ya Marekani inatumia vyombo vya kifedha kulazimisha majimbo kuoanisha sera zao za kibiashara na maslahi ya kisiasa ya Washington na Tel Aviv.
Masharti hayo yanaibua alama ya kuuliza kuhusu uhuru wa kuchukua maamuzi ya ndani na kupunguza nafasi ya ukosoaji na upinzani wa ndani kwa sera za kimataifa za Washington; suala ambalo linakinzana waziwazi na dhana ya mfumo wa Federali huko Marekani, ambao umejengeka kwenye msingi wa uhuru na mamlaka ya kiwango fulani ya majimbo ya nchi hiyo.
Katika mtazamo wa kijamii pia, sera za aina hii zinaweza kuwa na matokeo mabaya, ikiwa ni pamoja na kupanua pengo kati ya Serikali ya Federali na jamii za majimbo, hasa katika maeneo ambayo hisia za umma kuhusu suala la Palestina na uungaji mkono wa haki za binadamu huko Gaza ni kubwa. Sera hizi pia, kwa muda mrefu, zitadhoofisha imani ya umma kuhusu utekelezaji wa haki wa serikali.
Sambamba na hayo, athari mbaya za sera hizo zitaenea hadi kwenye ngazi ya kimataifa. Marekani daima imekuwa ikidai kutetea uhuru wa kujieleza, uhuru wa taasisi na jumuiya za kutetea haki za binadamu, lakini sera yake ya ndani inapotumika kuhudumia waziwazi maslahi ya mhusika wa kigeni, madai haya yanatiliwa shaka kwa urahisi katika duru za kimataifa.

Lakini swali kuu ni kwamba, kwa nini utawala wa Trump umepitisha sera hizo? Jibu liko katika uhusiano wa kina wa kiitikadi na kisiasa kati ya harakati za mrengo wa kulia nchini Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Tangu aingie madarakani, Trump amekuwa akifanya kila awezalo kuiridhisha lobi yenye nguvu inayoiunga mkono Israel nchini Marekani. Kuhamishia ubalozi wa Marekani mjini Baitul Muqaddas (Jerusalem), kukata msaada kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbiizi wa Kipalestina (UNRWA, na kutambua Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu kama sehemu ya eneo la Israel yote haya ni hatua zinazoendana na mkakati huu mkuu wa harakati za mrengo wa kulia nchini Marekani.
Tishio la sasa la Trump dhidi ya majimbo yanayounga mkono na kutetea Palestina pia linaweza kueleweka katika muktadha huu. Lengo ni kukandamiza sauti yoyote ya upinzani dhidi ya msaada usio na masharti wa Marekani kwa Israel, hata ndani ya ardhi ya Marekani.