Kupungua sana uungaji mkono wa Wamarekani kwa Israel, sababu na matokeo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129350
Himaya na msaada wa Marekani kwa Israel, kama mmoja wa washirika wake wa karibu, umekuwa mhimili mkuu wa sera za nje za Marekani kwa miongo kadhaa kutokana na masuala ya kisiasa, kihistoria na kimkakati.
(last modified 2025-08-10T02:30:02+00:00 )
Aug 10, 2025 02:30 UTC
  • Kupungua sana uungaji mkono wa Wamarekani kwa Israel, sababu na matokeo

Himaya na msaada wa Marekani kwa Israel, kama mmoja wa washirika wake wa karibu, umekuwa mhimili mkuu wa sera za nje za Marekani kwa miongo kadhaa kutokana na masuala ya kisiasa, kihistoria na kimkakati.

Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni, msaada na uungaji mkono wa Marekani kwa Israel umepungua kwa kiasi kikubwa kati ya maoni ya umma ya Marekani. Mabadiliko haya yanaonekana hasa miongoni mwa vizazi vipya na makundi makhsusi ya kisiasa, na yamechangiwa na matukio ya kikanda, siasa za ndani za Marekani, na mabadiliko ya maadili ya kijamii. Kura ya maoni ya hivi majuzi ya Gallup (iliyofanywa kati ya Julai 7 na 21, 2025) inaonyesha kwamba uungaji mkono kwa hatua za Israel huko Gaza umefikia kiwango cha chini kabisa cha asilimia 32 tu ya Wamarekani. Pia, ni asilimia 38 pekee waliounga mkono hatua za kijeshi za Israel dhidi ya Iran. Takwimu hizi zinaonyesha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa uungaji mkono wa Wamarekani kwa Israel ikilinganishwa na miongo iliyopita, wakati uungaji mkono huo ulikuwa wa zaidi ya 60%.

Miongoni mwa makundi ya umri, uungaji mkono kwa Israel umepungua kwas kiasi kikubwa sana kati ya vijana wa Marekani wenye umri wa miaka 18 hadi 34, na ni asilimia 9 pekee wanaounga mkono mauaji ya kimbari yanayofanyika huko Gaza. Hata kati ya wale wenye umri wa zaidi ya 55, uungaji mkono huo umeshuka chini ya 50%, kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa hapo kabla.

Utafiti mwingine wa Kituo cha Utafiti cha Pew uliofanyika mwaka huu wa 2025 uligundua kuwa asilimia 55 ya Wamarekani wana maoni hasi kuhusu Israel, ikilinganishwa na asilimia 41 mnamo 2020. Sababu za kupungua uungaji mkono wa Wamarekani kwa Israel nchini Marekani ni pamoja na kuongezeka uelewa wa umma kuhusu masuala ya haki za binadamu. Kuongezeka upatikanaji wa habari kupitia mitandao ya kijamii, picha na ripoti za vifo vya raia wa Kipalestina huko Gaza na Ukingo wa Magharibi, haswa watoto na wanawake, zimeimarisha hisia hasi miongoni mwa Wamarekani dhidi ya Israel. Kufichuliwa ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na Israel, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina na kushambuliwa na kulipuliwa kwa mabomu makazi ya raia, vimepelekea kupungua uhalali wa vitendo vya Israel kwenye macho na maoni ya umma.

Kwa upande mwingine, mabadiliko ya kijamii na kisiasa nchini Marekani yamechangia kupungua kwa uungaji mkono kwa Israel miongoni mwa baadhi ya Wamarekani. Vizazi vipya, haswa kile kinachojulikana kama Gen Z na millennials, vina maadili tofauti na ya vizazi vilivyotangulia na vinajali zaidi masuala ya uadilifu wa kijamii na haki za binadamu. Ukosoaji wa Israel kutokana na sera zake dhidi ya Wapalestina umeongezeka zaidi miongoni mwa Wanademokrati. Makundi haya yanaamini kuwa uungaji mkono usio na mpaka wa Marekani kwa Israel hauendani na maadili ya kidemokrasia.

Matukio ya kieneo na mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran pia yamekuwa na taathira katika kubadilisha mitazamo ya baadhi ya Wamarekani. Mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran mwezi Juni 2025 hasa katika maeneo ya makazi ya raia, vituo vya nyuklia na kijeshi nchini Iran, kwa msaada wa wazi na wa moja kwa moja wa Marekani, yameibua ukosoaji mkubwa katika nchi hiyo. Wamarekani wengi, haswa baada ya kuwekwa wazi vifo vya raia nchini Iran, waliutaja msaada huo kuwa sio wa lazima bali ni hatari.

Inatupasa pia kusema kuwa, mashinikizo za ndani nchini Marekani katika fremu ya mashindano ya uchaguzi, na ushawishi wa jamii za Waarabu na Waislamu katika majimbo muhimu kama vile Michigan vimeufanya uungaji mkono usio na masharti wa Marekani kwa Israel kuwa suala nyeti.

Hali hii ina taathira na matokeo hasi. Kwa mfano, kupungua uungwaji mkono wa umma kwa Israel kunaweza kuzidisha mashinikizo kwa wanasiasa wa Marekani kutazama upya misaada ya kijeshi na kifedha ya nchi hiyo kwa Tel Aviv. Suala hili linaweza kupelekea kupunguzwa msaada wa kila mwaka wa dola bilioni 3.8 kwa Israel au kuwekwa masharti magumu kwa ajili ya kupata msaada huo.

Askari wa Marekani wakikabiliana na wanafunzi wa vyuo vikuu wanaoipinga Israel huko Marekani

Kuongezeka hali ya kutengwa Israel katika jukwaa la kimataifa ni matokeo mengine ya kupungua uungaji mkono wa umma wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni. Kwa maneno mengine ni kuwa, kupungua uungaji mkono wa Marekani kama mtetezi na muungaji mkono mkuu wa Israel, kutapelekea utawala huo kutengwa zaidi katika jumuiya za kimataifa hasa kwa kuzingatia kuwa uungaji mkono kwa Israel barani Ulaya pia unapungua. Vilevile, kupungua himaya na uungwaji mkono wa Wamarekani kwa Israel kunaweza kuimarisha harakati kama vile BDS (ya kususia na kuweka vikwazo dhidi ya Israel) na kuongeza mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa kwa utawala huo.