Macron akiri ukandamizaji wa Ufaransa katika makoloni yake
-
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amekiri makosa ya nchi yake katika makoloni yake kabla, wakati na baada ya uhuru wa mataifa hayo ikiwemo Cameroon na Senegal.
Katika barua aliyomwandikia Rais Paul Biya wa Cameroon, kiongozi huyo wa Ufaransa amekubaliana na ripoti ya kamisheni ya wachunguzi wa kihistoria aliyoagiza kuchunguza maovu ya utawala wa Ufaransa kwa nchi hiyo na nyenginezo ila amekanusha madai ya maovu katika nchi ya Algeria.
Hii inafuatia ripoti ya pamoja ya wanahistoria wa Cameroon na Ufaransa iliyochunguza ukandamizaji wa Ufaransa wa harakati za uhuru kutoka 1945 hadi 1971.
Ripoti hiyo ya kamisheni ya wanahistoria imeeleza kuwa, Ufaransa ilifanya vitendo vya kikatili dhidi ya raia wa Cameroon ikiwemo kuwalazimisha kuyahama makaazi yao, kuwaweka maelfu katika kambi za vizuizi pamoja na kuunga mkono makundi ya wapiganaji waliojaribu kuzuia nchi hiyo kupata uhuru wake. Haya yalifanyika kati ya mwaka 1945 na 1971.
Lakini Macron hakuomba msamaha wazi kwa ukatili uliofanywa na wanajeshi wa Ufaransa katika koloni lake la zamani, ambalo lilipata uhuru mnamo 1960.
Kiongozi huyo wa Ufaransa aliwataja vigogo wanne wa kupigania uhuru waliouawa wakati wa operesheni za kijeshi zilizoongozwa na vikosi vya Ufaransa, akiwemo Ruben Um Nyobe, kiongozi shupavu wa chama cha kupinga ukoloni cha UPC.
Barua ya Macro ambayo aliituma wiki iliyopita kwa Rais Biya pia inaziorodhesha Rwanda na Senegal kuwa miongoni mwa nchi ambazo Ufaransa inakubali kusababisha maovu mengi kwa raia wao. Lakini rais huyo amekataa madai kwamba majeshi ya nchi yake yalifanya vitendo vya kikatili nchini, taifa la kaskazini mwa Afrika ililotawala kwa muda mrefu zaidi.