Waliokufa kwa maafa ya mafuriko Pakistan wapindukia 600
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129688-waliokufa_kwa_maafa_ya_mafuriko_pakistan_wapindukia_600
Idadi ya watu waliopoteza maisha kufuatia janga la mafuriko nchini Pakistan imeongezeka na kupindukia 600.
(last modified 2025-08-19T02:53:28+00:00 )
Aug 19, 2025 02:53 UTC
  • Waliokufa kwa maafa ya mafuriko Pakistan wapindukia 600

Idadi ya watu waliopoteza maisha kufuatia janga la mafuriko nchini Pakistan imeongezeka na kupindukia 600.

Kufuatia mvua za masika nchini Pakistan tangu Julai 25 mwaka huu, watu 657 wamepoteza maisha na karibu 1,000 wamejeruhiwa.

Wataalamu nchini Pakistan wamefananisha msimu wa mvua hizi za masika na mvua hatari na kuonya kuwa madhara ya mvua hizo zisizokwisha yanaathiri hali ya kijamii na maisha ya watu nchi hiyo.

Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Majanga ya Pakistan imetoa takwimu za hivi karibuni zaidi kuhusu vifo vya watu kufuatia mvua za masika na athari zake kama vile mafuriko, maporomoko ya ardhi, kukatwa kwa umeme na kuporomoka kwa paa za nyumba za makazi.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, katika kipindi cha chini ya miezi miwili (kuanzia Julai 25 hadi Agosti 15), watu wasiopungua 657 wamefariki dunia na 920 kujeruhiwa katika maeneo mbalimbali ya Pakistan, hasa majimbo ya Punjab na Khyber Pakhtunkhwa.

Maafisa wa Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Pakistan wanaendelea kuonya juu ya uwezekani wa kuendelea kunyesha mvua kubwa katika mikoa mbalimbali hasa maeneo yaliyoathirika.

Mvua za monsuni, ambazo kwa kawaida hunyesha kuanzia Juni hadi Septemba, mara nyingi husababisha hasara na uharibifu kote Asia Kusini, ikiwa ni pamoja na Pakistan, lakini katika miaka ya karibuni mabadiliko ya tabianchi yameongeza hali ya kutotabirika unyeshaji wake na nguvu yake.