Uhispania yataka Israel ifukuzwe kwenye mashindano ya baiskeli
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130472-uhispania_yataka_israel_ifukuzwe_kwenye_mashindano_ya_baiskeli
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania ameunga mkono wito wa kuondolewa timu ya waendesha baiskeli ya Israel kwenye mashindano ya mchezo huo yanayoendelea, kufuatia maandamano na malalamiko ya waungaji mkono wa Palestina nchini humo.
(last modified 2025-09-06T11:29:21+00:00 )
Sep 06, 2025 11:29 UTC
  • Uhispania yataka Israel ifukuzwe kwenye mashindano ya baiskeli

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania ameunga mkono wito wa kuondolewa timu ya waendesha baiskeli ya Israel kwenye mashindano ya mchezo huo yanayoendelea, kufuatia maandamano na malalamiko ya waungaji mkono wa Palestina nchini humo.

Akiongea kwenye idhaa ya Redio Nacional de Espana (RNE), Jose Manuel Albares ameeleza kutoridhishwa na ushiriki wa Israel kwenye mashindano hayo, akisisitiza kwamba ingawa anafadhilisha kutimuliwa kwa timu hiyo, lakini uamuzi wa mwisho ulikuwa wa Shirikisho la Kimataifa ya Uedeshaji Baiskeli (UCI), taasisi inayosimamia mchezo huo duniani.

Albares alitoa ridhaa yake ya kufukuzwa timu ya Waisraeli ya Israel–Premier Tech kwenye mashindano hayo ya 'Vuelta a Espana' ya 2025 mnamo Jumatano.

Matamshi yake yamekuja huku kukiwa na maandamano ya mara kwa mara ambayo yametatiza mashindano hayo, ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa duru ya 11 ya mashindano hayo huko Bilbao. Hapo awali, waandamanaji walizuia ushiriki wa Israel katika duru ya 5 ya mashindano hayo huko Figueres.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesisitiza kuwa, Uhispania haiwezi kuendeleza uhusiano wake na utawala wa Israel katika hali ya kawaida na kuongeza kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kutuma ujumbe wa wazi kwa Israel katika kukabiliana na mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Gaza.

Álbarez hivi karibuni alisisitiza haja ya kuchukuliwa hatua za adhabu dhidi ya utawala wa Kizayuni ili kuhakikisha unakomesha mashambulizi ya kijeshi huko Gaza na kusema kwamba "hadhi na itibari ya Ulaya iko hatarini kwa kufumbia macho jinai hizo.

Kabla ya hapo, Yolanda Diaz, Naibu Waziri Mkuu wa Pili wa Uhispania alisema katika taarifa yake kabla ya kushiriki katika maandamano ya kuunga mkono Palestina yaliyofanyika katika eneo la Praia America la Galicia, nchini Uhispania kuwa, "Kudumisha uhusiano wa kibiashara na makampuni ya Israel ni kuendeleza mauaji ya halaiki huko Palestina, na Umoja wa Ulaya pia lazima usitishe mikataba ya silaha na Israel."