Tuzo ya Amani ya FIFA kwa Trump yaitwa 'Joki ya Karne'
https://parstoday.ir/sw/news/world-i133990-tuzo_ya_amani_ya_fifa_kwa_trump_yaitwa_'joki_ya_karne'
Watumiaji wa mitandao ya kijamii wanasema kwamba hatua ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ya kumpa Tuzo ya Amani Rais Donald Trump wa Marekani ndio habari ya kipuuzi zaidi ambayo wamewahi kusikia maishani mwao.
(last modified 2025-12-06T13:06:43+00:00 )
Dec 06, 2025 13:06 UTC
  • Trump akipewa Tuzo ya Amani ya FIFA
    Trump akipewa Tuzo ya Amani ya FIFA

Watumiaji wa mitandao ya kijamii wanasema kwamba hatua ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ya kumpa Tuzo ya Amani Rais Donald Trump wa Marekani ndio habari ya kipuuzi zaidi ambayo wamewahi kusikia maishani mwao.

Wanaharakati wa kimataifa wametilia shaka uamuzi wa FIFA wa kumpa Trump Tuzo ya Amani na kuudhihaki kwa kuchapisha picha na michoro ya katuni.

Wakizungumzia jinsi Rais huyo wa Marekani alivyotuma silaha zinazotumiwa na Israel katika mauaji ya kimbari ya Wapaletina wa Ukanda wa Gaza, kutochukua kwake hatua za kivitendo za kuzuia vita vya Gaza kwa wakati mwafaka na mienendo yake mingine ya kivita dhidi ya nchi nyingine kama Venezuela, wadau wa mitandao ya kijamii wameitaja hatua ya FIFA kuwa ni mchezo wa kisiasa usiostahili heshima ya shirika la kimataifa.

Tuzo ya kwanza ya Amani ya FIFA ilitangazwa jana kwa mara ya kwanza, na kutolewa kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, wakati wa hafla ya droo ya Kombe la Dunia.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii pia wamekitaja kitendo cha FIFA kuwa ni kielelezo cha udhaifu na utegemezi wa shirikisho hilo la kimataifa la mpira wa miguu, wakisisitiza kwamba kumpa Tuzo ya Amani mtu kama Trump kumebakisha doa la fedheha na aibu katika kipaji cha FIFA. Vileve wametoa wito wa kususiwa mashindano ya Kombe la Dunia yanayofanyika mwakani.

Mmoja wa watumiaji wa mitandao ya kijamii amesema: Hatua ya FIFA kumpa Trump Tuzo ya Amani ni kichekesho cha karne.

Mdau mwingine wa mitandao ya kijamii amesema: Baada ya Trump kupewa Tuzo ya amani ya FIFA, huwenda pia Shirikisho la Soka Duniani likatoa tuzo hiyo kwa Wazayuni wa Israel kwa kuwaua watu wa Wapalestina!

Mtumiaji mwingine ameandika: "Dunia hii inaonekana kutawaliwa na watu wakatili. Sasa tuzo hazitolewi kwa msingi wa kutenda wema, bali kwa msingi wa maslahi na faida. Haijalishi anayepewa ni muovu kiasi gani, atapewa tuzo alimradi tu ana faida na maslahi..."