Human Rights Watch: Haki ya kuandamana inahujumiwa nchini Uingereza
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema jana Alhamisi kwamba haki ya kuandamana nchini Uingereza inahujumiwa baada ya kupitishwa hatua za ukandamizaji ambazo zimezidisha masharti na adhabu dhidi ya maandamano ya amani.
Katika ripoti yenye kichwa cha habari "Kunyamazisha Mitaa: Haki ya Kuandamana Inashambuliwa nchini Uingereza," shirika hilo la kutetea haki za binadamu limelaani utekelezaji wa "vikwazo vya demokrasia" dhidi ya haki ya kuandamana, jambo ambalo ni ukiukaji wa majukumu ya kimataifa ya nchi hiyo kuhusu haki za binadamu.
"Tunashuhudia mmomonyoko wa haki za msingi za kidemokrasia ... na hili lazima likomeshwe," amesema Yasmin Ahmed, mkurugenzi wa Human Rights Watch nchini Uingereza.
Shirika hilo limeeleza masikitiko yake kwamba serikali ya chama cha Labour, inayoongozwa na Keir Starmer - ambaye aliingia madarakani mwaka 2024 - haikufuta sheria mbili zilizopitishwa na serikali za Conservative mnamo 2022 na 2023, ambazo zilipunguza kizingiti cha kufafanua kosa la kuvuruga nidhamu ya umma ili kurahisisha kukamatwa, au kuruhusu kukamatwa waandamanaji.
Sheria hizo mbili zilipitishwa kufuatia maandamano yaliyoongezeka ya makundi ya kutetea mazingira ya Extinction Rebellion na Just Stop Oil.
Awali, Amnesty International ilikuwa imelaani ukatili wa polisi wa Uingereza dhidi ya waandamanaji mwezi Septemba mwaka jana, ikisema kwamba kukamatwa kwa mamia ya waandamanaji wanaounga mkono Palestina ni ukiukaji wa sheria za kimataifa, ikisisitiza kwamba "kujinaisha kitendo cha kuinua bendera ya amani ni ukiukaji mkubwa wa uhuru wa kujieleza."
Inafaa kukumbusha kwamba mwezi Julai mwaka jana Uingereza ilipiga marufuku kundi la "Palestine Action" ambalo ni moja ya mashirika makubwa zaidi ya Uingereza yanayowaunga mkono Wapalestina.