Russia yashambulia viwanda vya kuunda droni  za kijeshi nchini Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135288-russia_yashambulia_viwanda_vya_kuunda_droni_za_kijeshi_nchini_ukraine
Jeshi la Russia, katika kujibu hujuma ya Ukraine dhidi ya makao ya Rais Vladimir Putin, limetekeleza mashambulizi kadhaa dhidi ya vituo vya kuunda ndege za kivita zisizo na rubani au droni nchini Ukraine.
(last modified 2026-01-09T07:33:02+00:00 )
Jan 09, 2026 07:33 UTC
  • Russia yashambulia viwanda vya kuunda droni  za kijeshi nchini Ukraine

Jeshi la Russia, katika kujibu hujuma ya Ukraine dhidi ya makao ya Rais Vladimir Putin, limetekeleza mashambulizi kadhaa dhidi ya vituo vya kuunda ndege za kivita zisizo na rubani au droni nchini Ukraine.

Kwa mujibu wa televisheni ya Russia ya RT, Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa vikosi vyake vimeshambulia kwa makombora dhidi ya viwanda hivyo muhimu vya Ukraine.

Taarifa hiyo imesema viwanda vilivyolengwa vilitumika katika kuunda droni ambazo zilitumiwa na utawala wa Ukraine kushambulia makao ya Rais Putin hivi karibuni.

Hivi karibuni Rais Vladimir Putin wa Russia alisema kuwa Moscow iko tayari kutumia nguvu za kijeshi kufikia malengo ya operesheni yake maalumu ya kijeshi iwapo Ukraine itaendelea kuchelewesha mazungumzo ya amani.

Rais wa Russia ameeleza kuwa viongozi wa Ukraine hawapigi hatua kuelekea kwenye ufumbuzi wa amani na kuongeza kusema: "Hilo tunalishuhudia hata leo hii, kwa bahati mbaya viongozi wa serikali ya Kiev hawana haraka ya kutatua mzozo huu kwa njia ya amani. Nilizungumzia suala hili mwaka mmoja uliopita katika hotuba yangu  kwenye Wizara ya Mambo ya Nje.

Mgogoro wa Ukraine ulioanza mwaka 2022 umefuatiwa na  ya uingiliaji wa kisiasa na kijeshi wa nchi za Magharibi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo, hatua ambayo Moscow inaaamini inayumbisha usalama katika maeneo ya karibu na mipaka ya Russia na kutishia usalama wa nchi hiyo.