Medvedev 'amdhihaki' Trump: Usipoharakisha, Greenland itapiga kura ya kujiunga na Russia
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Russia Dmitry Medvedev amesema, Wagreenland wanaweza kupiga kura ya maoni ya kujiunga na Russia ikiwa Rais wa Marekani Donald Trump hatachukua hatua haraka kukinyakua kisiwa hicho cha ncha ya kaskazini, Aktiki.
"Trump anapaswa afanye haraka. Kwa mujibu wa taarifa ambazo hazijathibitishwa, ndani ya siku chache inaweza kuwepo kura ya maoni ya ghafla, ambapo Greenland nzima yenye watu 55,000 inaweza kupiga kura kujiunga na Russia," shirika la habari la Interfax limeripoti, likimnukuu Medvedev, ambaye ni rais wa zamani wa Russia akitoa kauli hiyo ambayo imetafsiriwa kuwa ni ya kumdhihaki rais wa Marekani ambaye ameonyesha kuwa na uchu mkubwa wa kukinyakua kisiwa hicho.
"Na hivyo ndivyo itavyokuwa. Hakutakuwa na nyota mpya kwenye bendera (ya Marekani)", ameeleza Medvedev kumaanisha nia ya Washington ya kulifanya eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali za madini kuwa jimbo la 51 la Marekani.
Trump amefufua upya takwa lake la kuhakikisha Marekani inaidhibiti Greenland, eneo la Denmark linalojiendeshea mambo yake ya ndani, akisema, Washington inahitaji kulimiliki eneo hilo ili kuzuia lisinyakuliwe na Russia na China. Rais wa Marekani amesema, Greenland na rasilimali zake ni muhimu kwa usalama wa taifa wa Marekani, msimamo ambao unapingwa vikali na Denmark na Greenland yenyewe.
Wakati Russia haijatoa tamko rasmi hadi sasa kuhusu madai hayo ya Trump, China kupitia msemaji wake wa Wizara ya Mambo ya Nje Mao Ning imelaani tuhuma hizo alizotoa rais wa Marekani ikisema, "ni kisingizio cha kufanikisha maslahi yake binafsi".
Mao ameuambia mkutano na waandishi wa habari kwamba, Aktiki "ina taathira kwa maslahi ya pamoja ya jamii ya kimataifa" na kwamba shughuli za Beijing katika eneo hilo "zinaimarisha amani, utulivu na maendeleo endelevu kwa mujibu wa sheria za kimataifa".../