Trump auza viti vya 'Bodi ya Amani' Gaza dola bilioni 1
Rais wa Marekani, Donald Trump amezitaka nchi mbali mbali duniani zilipe angalau dola bilioni 1 ili kusalia katika "Bodi ya Amani" ya Gaza, baada ya kumalizika muhula ulioanishwa wa miaka mitatu.
Mapema wiki hii, Ikulu ya White House ilizindua rasmi Awamu ya Pili ya 'mpango wa amani' Gaza unaosimamiwa na Marekani, na kuanzisha kile kinachoitwa 'Bodi ya Amani' ili kusimamia ujenzi mpya wa eneo hilo la Wapalestina linalokaliwa kwa mabavu.
Inaripotiwa kwamba, hati inayoelezea muundo wa bodi hiyo na masharti ya uanachama imesambazwa, huku mialiko ikitumwa kwa viongozi kadhaa wa dunia, ikiwaomba kujiunga na jopo hilo.
"Kila nchi mwanachama itahudumu kwa muhula usiozidi miaka mitatu baada ya Mkataba huu kuanza kazi, na muhula huo unaweza kutazama upya na Mwenyekiti," hati hiyo imesema.
"Muhula wa uanachama wa miaka mitatu hautatumika kwa nchi wanachama zinazochangia zaidi ya dola za Kimarekani $1,000,000,000 (bilioni 1) kama fedha taslimu kwa Bodi ya Amani ndani ya mwaka wa kwanza wa Mkataba kuanza kazi."
Orodha ya wasimamizi wa bodi hiyo inajumuisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mark Rubio, mjumbe maalumu wa Trump eneo la Asia Magharibi, Steve Witkoff, mkwe wa Trump Jared Kushner, na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, viongozi wengine walioalikwa kujiunga na bodi hiyo ni pamoja na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney, na Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva.