'Bodi ya Amani' ya Trump ni aina ya ukoloni mamboleo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135786-'bodi_ya_amani'_ya_trump_ni_aina_ya_ukoloni_mamboleo
Mkuu wa Jamaat-e-Islami Pakistan (JIP) ametangaza kwamba "Bodi ya Amani" iliyotangazwa na Rais wa Marekani, Donald Trump kusimamia utawala wa eneo la Palestina la Ukanda wa Gaza ni aina mpya ya mfumo wa ukoloni mamboleo. Bodi hiyo ni taasisi inayojumuisha watu kama Tony Blair, mmoja wa wahusika wakuu wa mauaji ya mamilioni ya watu wa Iraq.
(last modified 2026-01-22T23:51:31+00:00 )
Jan 22, 2026 23:51 UTC
  • 'Bodi ya Amani' ya Trump ni aina ya ukoloni mamboleo
    'Bodi ya Amani' ya Trump ni aina ya ukoloni mamboleo

Mkuu wa Jamaat-e-Islami Pakistan (JIP) ametangaza kwamba "Bodi ya Amani" iliyotangazwa na Rais wa Marekani, Donald Trump kusimamia utawala wa eneo la Palestina la Ukanda wa Gaza ni aina mpya ya mfumo wa ukoloni mamboleo. Bodi hiyo ni taasisi inayojumuisha watu kama Tony Blair, mmoja wa wahusika wakuu wa mauaji ya mamilioni ya watu wa Iraq.

Hafiz Naeem ur Rehman amesisitiza katika ujumbe wake kwamba bodi hiyo ni chombo kipya cha kunyakua rasilimali na ardhi za Palestina, na kwamba jaribio lolote la kulazimisha utawala wa Marekani juu ya eneo la Gaza kwa kisingizio cha "ujenzi mpya" halikubaliki kabisa.

Ameongeza kuwa: "Madai ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan kwamba nchi hiyo inaunga mkono mpango wa usalama na amani wa Gaza chini ya azimio la Baraza la Usalama hayaendani na ukweli."

Mkuu wa Jamaat-e-Islami Pakistan amesema, Donald Trump mwenyewe amesema waziwazi kwamba "bodi yake ya amani" inaweza siku moja kuchukua nafasi ya Umoja wa Mataifa. Kwa kuzingatia msimamo huu, haiwezekani kutetea msimamo wa Pakistan wa kujiunga na chombo kama hicho.

Hafiz Naeem ur Rehman amemalizia kwa kusema: "Tunasema tena wazi kwamba jeshi la Pakistani halipaswi kutumwa Gaza kwa hali yoyote ile."

Trump alitangaza kuundwa chombo hicho kinachoitwa 'Bodi ya Amani' ya Gaza siku ya Ijumaa, akisema  wajumbe wa baraza hilo watatambulishwa hivi karibuni.