Maelfu waandamana Australia kupinga ziara ya rais wa utawala wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136498-maelfu_waandamana_australia_kupinga_ziara_ya_rais_wa_utawala_wa_israel
Ziara rasmi ya rais wa utawala wa Israel, Isaac Herzog, nchini Australia ilikumbwa na maandamano makubwa siku ya Jumatatu, huku maelfu ya waandamanaji wakijitokeza katika miji kadhaa, hali iliyopelekea kuwepo makabiliano na polisi.
(last modified 2026-02-11T07:02:56+00:00 )
Feb 11, 2026 07:02 UTC
  • Maelfu waandamana Australia kupinga ziara ya rais wa utawala wa Israel

Ziara rasmi ya rais wa utawala wa Israel, Isaac Herzog, nchini Australia ilikumbwa na maandamano makubwa siku ya Jumatatu, huku maelfu ya waandamanaji wakijitokeza katika miji kadhaa, hali iliyopelekea kuwepo makabiliano na polisi.

Herzog alianza ziara ya siku nne kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, ziara iliyoelezwa kuwa ni ishara ya mshikamano na jamii ya Kiyahudi kufuatia shambulio la tarehe 14 Desemba katika eneo la Bondi Beach mjini Sydney, lililosababisha vifo vya watu 15.

Hata hivyo, ziara hiyo imezua mjadala na upinzani mkubwa, huku wanaharakati wakimtuhumu Herzog kwa kuhusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala katili wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. Maandamano yaliyojumuisha maelfu ya watu yalifanyika kwa wakati mmoja katika miji na vitongoji mbalimbali, yakiwemo ya Sydney, ambako maelfu walikusanyika katika eneo la biashara katikati ya jiji (CBD), wakisikiliza hotuba na kupaza sauti zenye kuunga mkono wananchi wa Palestina.

Mmoja wa waandamanaji, Jackson Elliott, mwenye umri wa miaka 30, alisema kuwa shambulio la Bondi lilikuwa “la kutisha sana,” lakini akaeleza masikitiko yake kwamba viongozi wa Australia wameshindwa kutambua na kuzungumzia ipasavyo mateso ya wananchi wa Palestina huko Gaza. Alimtuhumu Herzog kwa kukwepa maswali yanayohusu Israel inavyokalia kwa mabavu wa ardhi za Palestina, akisisitiza kuwa ziara hiyo haipaswi kuonekana kama suala la kawaida la mahusiano ya kidiplomasia pekee.

Katika mji wa Sydney, kulishuhudiwa ulinzi mkali, ukiwemo uwepo wa polisi wapanda farasi na ufuatiliaji wa anga. Mamlaka zilisema takribani maafisa 3,000 wa polisi walihusishwa katika operesheni ya kiusalama wakati wa ziara hiyo.

Polisi walitumia pilipili  na gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakijaribu kuvunja vizuizi vya kiusalama, jambo lililosababisha makabiliano na kukamatwa kwa watu kadhaa. Baadhi ya waandishi wa habari pia waliripotiwa kuathiriwa na pilipili manga wakati wa vurugu hizo.

Kwa mujibu wa wachambuzi, matukio haya yanaakisi hisia zinazozidi kuongezeka miongoni mwa jamii mbalimbali kuhusu suala la Palestina na jinai zinazotekelezwa na utawala dhalimu wa Israel katika eneo hilo.