Mamilioni ya dola zatumika kwenye kampeni za uchaguzi wa rais Marekani
Vyombo vya habari vya Marekani vimefichua matumizi makubwa kupindukia ya fedha katika kampeni za uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.
Huku kampeni za uchaguzi wa rais zikiwa zinaendelea, vyombo vya habari vya Marekani vimetangaza kuwa Hillary Clinton, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democrats alitumia karibu dola milioni 38 katika mwezi uliopita; naye Donald Trump anayewania kiti hicho kupitia chama cha Republican ametumia dola milioni 18.5.
Wakati huohuo kanali ya televisheni DW ya Ujerumani imeripoti kuwa si mashirika ya Kimarekani pekee yanayowekeza kwenye uchaguzi wa Marekani bali mashirika ya Ulaya na ya nchi za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia yanawekeza katika uchaguzi huo.
Suala la gharama zinazotumiwa katika uchaguzi wa Marekani na mchango unaotolewa na baadhi ya nchi kugharamia kampeni za uchaguzi ikiwemo Saudia limezusha makelele na kuakisiwa na vyombo vya habari vya Marekani.
Tovuti ya Shirika rasmi la habari la Jordan iliripoti kwa kumnukuu Mwanamfalme Muhammad bin Salman wa utawala wa Aal Saud kwamba Saudia imekubalia kugharamia asilimia 20 ya fedha za kampeni za Hillary Clinton, lakini baada ya saa chache habari ilifutwa kwenye tovuti ya shirika hilo.
Habari za kukithiri matumizi ya pesa za kampeni katika uchaguzi wa rais wa Marekani zinatolewa katika hali ambayo wagombea wakuu wa uchaguzi huo Hillary Clinton wa Democrats na Donald Trump wa Republican wanaendelea kuwashawishi wapiga kura washiriki kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 8 mwaka huu huku kila mmoja akijaribu kuonyesha kuwa mgombea mwenzake hana ustahiki wa kushika wadhifa wa urais wa nchi hiyo.../