Medvedev: Mashambulizi dhidi ya Iran ni uchokozi unaokiuka misingi ya uungwana
-
Dmitry Medvedev
Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama la Russia ametuma ujumbe akimpongeza Kiongozi Mkuu mpya wa Iran, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei na kusema kuwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya ardhi ya Iran ni uchokozi unaokiuka misingi ya uungwana na wala hayawezi kuhalalishwa kwa njia yoyote.
Katika ujumbe wake kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Mojtaba Khamenei, uliochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, Dmitry Medvedev amesema: "Kwa heshima, pokea pongezi zangu za dhati kwa kuchaguliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."
Katika ujumbe huo, Medvedev amesisitiza udharura wa kudumishwa ushirikiano wa Russia na Iran na kusema: "Nina imani kwamba Russia na Iran zitaendeleza ushirikiano wao athirifu licha ya mashinikizo ya kigeni."
Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama la Russia ameongeza kuwa, "ninaliombea taifa la Iran liendelee kusimama imara na kishujaa katika mapambano ya kupigania mamlaka ya nchi yao."
Ayatullah Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei alichaguliwa tarehe 9 mwezi huu wa Machi kuwa Kiongozi Mkuu mpya wa Iran baada ya mtangulizi wake, Ayatullah Ali Khamenei, kuuawa shahidi katika shambulizi la kigaidi la Marekani na Israel, akiwa pamoja na watu kadhaa wa familia yake akiwemo mke na mjukuu wake.