Guardian: Iron Dome imeshindwa kukabiliana na makombora ya Iran
Gazeti la The Guardian la Uingereza limeandika katika ripoti inayozungumzia kushindwa kwa Iron Dome katika kukabiliana na makombora ya Iran kwamba: "Mng’aro wa makombora madogo magogo angani nyakati za usiku limekuwa jambo la kawaida kwa Waisraeli, huku Iran ikiendelea kutumia vyema udhaifu wa ulinzi wa anga wa utawala wa Israel."
Ripoti ya The Guardian inasema: Kombora la Khorramshahr, ambalo ni mojawapo ya makombora ya kisasa zaidi ya balestiki ya Iran, linaaminika kuwa na uwezo wa kubeba kichwa cha mlipuko kinachosambaza hadi mabomu 80 ya wastani kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tangu kuanza kwa Vita vya Ramadhani, makombora ya Khorramshahr yamekuwa yakiunyima usingizi utawala wa Israel, ambao una mfumo wa ulinzi wa makombora wenye tabaka kadhaa na unaodaiwa kuwa tata na wa kisasa zaidi duniani.
Ripoti ya gazeti la The Guardian la Uingereza inaeleza kuwa tangu kuanza Vita vya Ramadhani, kwa uchache makombora 19 ya balestiki yenye vichwa kadhaa vya milipuko yamevuka salama mfumo wa Iron Dome na kulenga shabaha kikamilifu, na kuongeza: "Mashambulizi haya yanaonyesha mabadiliko makubwa katika mbinu za Iran, ambazo zimefichua udhaifu wa ulinzi wa anga wa utawala wa Israel."
Awali, televisheni ya al Jazeera ya Qatar ilikuwa imetangaza katika ripoti ya uchambuzi kwamba kuingia mabomu yenye vichwa kadhaa vya milipuko na makombora mapya ya Iran kwenye uwanja wa vita kumeuingiza mzozo kati ya Tehran na Tel Aviv katika hatua ngumu zaidi na kuzua maswali mazito kuhusu ufanisi wa mifumo ya ulinzi wa anga ya Israel.
Mtandao wa al Jazeera umesisitiza kwamba mabadiliko ya mbinu za Iran yanaonesha "mabadiliko ya ubora" katika aina ya mashambuliziya Jamhuri ya Kiislamu.