Iran yataka Umoja wa Mataifa uwalaani wavamizi na uwawajibishe
-
Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Aragchi (kulia) na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za dhati na kutoa msimamo thabiti na wa wazi katika kulaani tawala zilizoanzisha vita dhidi ya Iran. Aidha ametaka uwezo wa taasisi hiyo na nchi huru utumike kuwawajibisha wahusika wa vita hivyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB, likinukuu tovuti ya taarifa ya serikali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Aragchi alifanya mazungumzo ya simu siku ya Alhamisi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.
Katika mazungumzo hayo ya simu, walijadili hali ya hivi karibuni ya eneo hilo pamoja na athari za kiusalama na kibinadamu zilizotokana na uvamizi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemjulisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu matukio ya karibuni pamoja na vitendo vya uhalifu vinavyoendelea kufanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni.
Araghchi amesisitiza azma na dhamira thabiti ya Iran ya kuendelea kujilinda kwa mujibu wa haki ya kujihami ili kulinda usalama wa taifa, mamlaka ya kitaifa na mipaka ya Iran.
Akizungumza kuhusu mashambulizi ya kikatili yanayoendelezwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya malengo ya kiraia, zikiwemo shule, hospitali, majengo ya kitamaduni na kihistoria, maeneo ya umma na vitongoji vya makazi, Araghchi amrkumbusha wajibu wa Umoja wa Mataifa na wa Katibu Mkuu wake katika kufuatilia ukiukaji mkubwa wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, ikiwemo haki za binadamu na sheria za kibinadamu, unaofanywa na wavamizi.
Araghchi pia amekosoa misimamo na wito wa upande mmoja kutoka kwa baadhi ya wahusika wanaoitaka Iran ijizuie na kusitisha vita, akisema haipaswi kupuuza ukweli ulio wazi kwamba Marekani, kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel, ilikiuka tena diplomasia na kuhatarisha usalama na maslahi ya nchi zote za eneo la Asia Magharibi kwa kuanzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iran na hivyo kulazimisha vita kwa eneo hilo na dunia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hali ya kutokuwa na usalama katika Lango-Bahari la Hormuz ni matokeo ya moja kwa moja ya ukiukaji wa sheria na uvamizi wa Marekani na utawala wa Kizayuni. Amesisitiza kwamba kuzuia kupita kwa meli zinazomilikiwa au zinazohusiana na maadui na washirika wao ni haki ya kisheria ya Iran kama taifa la pwani. Ameongeza kuwa mamlaka husika za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimechukua hatua zinazofaa kwa kutambua wajibu wao wa kuhakikisha usalama katika njia hiyo muhimu ya baharini.
Waziri huyo pia amesisitiza tena haja ya Umoja wa Mataifa kuchukua hatua madhubuti na kutoa msimamo wazi katika kutekeleza jukumu lake la msingi la kulinda amani na usalama wa kimataifa kwa kulaani wavamizi na kutumia uwezo wa taasisi hiyo pamoja na nchi huru ili kuwawajibisha wanaovuruga usalama.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza msimamo wa kimsingi wa Umoja wa Mataifa kuhusu umuhimu wa kuheshimu mamlaka ya kitaifa na mipaka ya nchi. Pia amebainisha wasiwasi mkubwa wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuendelea kwa vita na mauaji katika eneo la Asia Magharibi.
Antonio Guterres aidha ametangaza kumteua Jean Arnault kuwa mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya Mashariki ya Kati, akisema lengo la uteuzi huo ni kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na maafisa wa Iran pamoja na kufanya mashauriano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kusaidia kutafuta suluhisho la mgogoro huo.