Sababu ya kujiuzulu Mkurugenzi wa Intelijensia ya Kitaifa wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i138580-sababu_ya_kujiuzulu_mkurugenzi_wa_intelijensia_ya_kitaifa_wa_marekani
Kuibuka kwa baadhi ya tofauti kati ya Rais wa Marekani na mkuu wa jumuiya ya ujasusi ya nchi hiyo kumezua shaka kuwa kujiuzulu kwa Tulsi Gabbard kulitokana na sababu za kisiasa.
(last modified 2026-05-23T13:17:14+00:00 )
May 23, 2026 13:14 UTC
  • Sababu ya kujiuzulu Mkurugenzi wa Intelijensia ya Kitaifa wa Marekani

Kuibuka kwa baadhi ya tofauti kati ya Rais wa Marekani na mkuu wa jumuiya ya ujasusi ya nchi hiyo kumezua shaka kuwa kujiuzulu kwa Tulsi Gabbard kulitokana na sababu za kisiasa.

Gabbard alijiuzulu Ijumaa kutoka nafasi yake ya Mkurugenzi wa Intelijensia ya Taifa, taasisi ya juu zaidi ya masuala ya usalama nchini Marekani, ambayo mkurugenzi wake anasimamia mashirika kumi na sita ya ujasusi na usalama nchini humo.

Katika barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Donald Trump wa Marekani, Gabbard ametaja ugonjwa hatari wa mumewe kuwa sababu ya kujiuzulu kwake na kusema kwamba anataka kumtunza kwa karibu katika wiki na miezi ijayo. Kwa maneno mengine, sababu kuu ya kujiuzulu kwa afisa huyo wa juu zaidi wa ujasusi na usalama wa Marekani ni suala la kibinafsi.

Hata hivyo, baadhi ya hitilafu kati ya rais wa Marekani na mkuu huyo wa zamani wa jumuiya ya ujasusi ya Marekani zimeibua mashaka kuwa kujiuzulu kwake kutokana na masuala ya kisiasa. Moja ya tofauti kuu kati ya Trump na Gabbard ni kuhusu suala la mpango wa amani wa nyuklia wa Iran. Kabla ya shambulio la Marekani dhidi ya Iran mwezi Juni mwaka jana, vilivyojulikana kama Vita vya Siku Kumi na Mbili, Gabbard alisema katika kikao cha Bunge la Congress kwamba kutokana na taarifa zilizokusanywa na jumuiya ya kijasusi ya Marekani Iran haikuwa na nia ya kutengeneza silaha za nyuklia na kwamba shughuli zake za nyuklia hazikuwa tishio kwa usalama wa Marekani. Msimamo huu wakati huo ulionekana kuwa uliokinzana na madai ya Trump kwamba Iran ilikuwa inataka kutengeneza silaha za nyuklia na kuonya kuwa Iran ingeshambuliwa kama Tehran haingetekeleza matakwa ya Marekani.

Katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa huko nyuma, Trump hata alimtuhumu afisa huyo wa juu zaidi wa ujasusi wa Marekani kwa kutofahamu mpango wa nyuklia wa Iran.

Bila shaka, Gabbard baadaye alijaribu kuepuka ghadhabu ya Trump kwa kubadilisha misimamo yake ya awali kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran kwa njia ambayo ingemridhisha rais wa Marekani. Hata hivyo, baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani viliendelea kuripoti kuwepo tofauti za msingi kati ya Trump na mkuu huyo wa jumuiya ya kijasusi ya Marekani.

Tofauti hizi hazikuishia tu kwa mkuu wa idara ya intelijensia ya Marekani. Wakati wa shambulio la kichokozi la Marekani na Israel mwezi Februari, linalojulikana kama Vita vya Siku Arubaini, dhidi ya Iran, mkuu wa Ofisi ya Kupambana na Ugaidi ya utawala wa Trump alijiuzulu katika kupinga vita hivyo. Hii ni katika hali ambayo upinzani dhidi ya shambulio haramu na lisiloidhinishwa la Marekani dhidi ya Iran haukufanywa tu na wanachama wa Democrat wa Congress ya Marekani, bali pia na baadhi ya Warepublican. Kwa mfano, wiki iliyopita, kwa mara ya kwanza na baada ya majaribio kadhaa yaliyofeli, Seneti inayodhibitiwa na Warepublican hatimaye iliidhinisha hatua ya kwanza ya kubana uwezo wa Trump kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran bila kupata idhini ya Congress. Katika Baraza la Wawakilishi, linalodhibitiwa na chama cha Trump pia, kura katika ukumbi huo pia iliahirishwa baada ya spika kuingilia kati na kuzuia hatua hiyo kumdhalilisha kisiasa Trump kuhusiana na suala hilo.

Kwa kuzingatia uzoefu huo, madai ya kujiuzulu Mkurugenzi wa Intelijensia ya Kitaifa wa Marekani kutokana na masuala binafsi yanatiliwa shaka kubwa.