Sababu za kuongezeka mgawanyiko barani Ulaya kuhusu utawala wa Kizayuni
Mbali na maoni ya wananchi, baadhi ya wabunge wa Bunge la Ulaya pia wameutaka Umoja wa Ulaya uchukue hatua kali dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na viongozi wake.
Ni wazi kuwa Umoja wa Ulaya hauna sera thabiti kuhusu utawala wa Kizayuni. Baadhi ya nchi zinaendelea kuunga mkono jinai za utawala huo ghasibu, huku nyingine zikitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya jinai zake. Hivi karibuni, José Manuel Álvarez, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania alisema: "Itamar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Israel, amepigwa marufuku kuingia Uhispania."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa pia alisema ataungana na mwenzake wa Italia katika kutoa wito kwa Umoja wa Ulaya umuwekee vikwazo Ben-Gvir; Waziri wa Usalama wa Ndani wa Israel na kumpiga marufuku kuingia katika nchi za Ulaya. Wabunge kadhaa wa Bunge la Ulaya pia wameutaka umoja huo uuwekee vikwazo utawala wa Kizayuni na wakati huo huo kukosoa kimya cha Umoja huo kuhusu jinai zinazofanywa na utawala huo wa kigaidi dhidi Wapalestina, mataifa ya eneo na wanaharakati wa misaada ya kibinadamu.
Swali ni je, ni sababu gani zimepelekea kuongezeka mgawanyiko barani Ulaya kuhusiana na utawala wa Kizayuni?
Hatua za kinyama za Israel dhidi ya wanaharakati wanaozuiliwa kwenye msafara wa meli za kimataifa za as-Sumud kuelekea Gaza zinaonekana kuibua mpasuko kati ya nchi hizo. Siku ya Jumatano, Itamar Ben-Gvir alichapisha video kwenye mitandao ya kijamii iliyomwonyesha akikejeli na kuwarushia matusi wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina ambao walikuwa wamefungwa pingu na kulazimishwa kupiga magoti na kushikiliwa katika maji ya kimataifa baada ya kukamatwa na majeshi ya Israel. Waziri wa mambo ya nje wa Uhispania ametaja mambo aliyowatendea waziri huyo wa Israel wanaharakati wanaozuiliwa kwenye msafara huo wa kimataifa kama sababu kuu ya kumpiga marufuku kuingia Uhispania. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa pia amelaani hatua ya kiharamia ya waziri huyo mbaguzi wa rangi.
Jambo jingine muhimu ni kwamba, watawala wa Israel hawajakabiliwa na adhabu yoyote ya kisheria na wamekuwa na kinga ya kuadhibiwa licha ya kufanya jinai chungu mzima dhidi ya binadamu, jinai za kivita na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza. Kutokana na kura za turufu za Marekani, Ufaransa na Uingereza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, baraza hilo limeshindwa kupitisha azimio lolote la maana dhidi ya utawala wa Kizayuni. Hali hii na kushindwa jamii ya kimataifa kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni kumeibua ghadhabu na hasira miongoni mwa raia wa kawaida na wanasiasa huru kimataifa.
Barry Andrews, Mbunge wa Bunge la Ulaya kutoka Ireland, amesema: "Umoja wa Ulaya unapaswa kumuwekea vikwazo mara moja Ben-Gvir na kusimamisha makubaliano ya ushirikiano kati ya umoja huo na Israel. Je, Berlin na Rome zitaendelea kuzuia hatua ya Umoja wa Ulaya dhidi ya utawala huo hadi lini? Ni wazi kuwa mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita unaendelea kufanywa na utawala huo wa kibaguzi bila kikomo na bila aibu yoyote. Jambo jingine muhimu ni ubaguzi wa rangi uliokithiri unaofanywa hadharani na serikali ya Netanyahu. Hatua ya Ben Gvir ya kukejeli na kuwatusi wanaharakati wa msafara wa meli za kimataifa za as-Sumud ni mfano wa wazi wa ubaguzi huu wa rangi. Billy Keller, Mbunge wa Bunge la Ulaya kutoka Ireland, amesema: "Israel, chini ya Netanyahu na Ben-Gvir, ni utawala wa itikadi kali na wa kibaguzi. Wanafanya vitendo vya kinyama dhidi ya watu wa Palestina ambavyo vinakiuka wazi sheria za kimataifa za kibinadamu. Matjaž Nemec, Mbunge wa Slovenia pia amesema video ya Ben-Gvir ni ishara ya siasa za kimfumo ambazo zinahitaji kukabiliwa na jibu kali la Ulaya.
Nukta ya mwisho ni kwamba, radiamali ya baadhi ya wabunge wa Bunge la Ulaya inatokana pia na ukweli kwamba Umoja wa Ulaya umejiletea aibu na kujipunguzia itibari wenyewe kutokana na kimya chake mbele ya jinai za utawala wa Kizayuni na viongozi wake wahalifu dhidi ya Wapalestina. Jambo muhimu ni kwamba hata kama radiamali hizo zinaashiria mwanzo wa harakati ya kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni, lakini ni wazi kuwa hazitarejesha itibari na sifa zilizopotea za Umoja wa Ulaya na nchi za Magharibi.