Wanaharakati London na Berlin walaani marufuku ya vazi la Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i14025-wanaharakati_london_na_berlin_walaani_marufuku_ya_vazi_la_kiislamu
Wanaharakati wanaopinga vitendo vya chuki dhidi ya dini ya Kiislamu wamefanya maandamano katika miji ya London na Berlin kulaani marufuku vazi la Kiislamu katika pwani za Ufaransa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 26, 2016 22:16 UTC
  • Wanaharakati London na Berlin walaani marufuku ya vazi la Kiislamu

Wanaharakati wanaopinga vitendo vya chuki dhidi ya dini ya Kiislamu wamefanya maandamano katika miji ya London na Berlin kulaani marufuku vazi la Kiislamu katika pwani za Ufaransa.

Nchini Uingereza waandamanaji wamefanya maandamano mbele ya ubalozi wa Ufaransa mjini London na kupiga nara dhidi ya siasa za uhasama za Paris dhidi ya dini ya Kiislamu nchini humo.

Wanawake wa Kiislamu katika maandamano ya mjini London

Katika maandamano hayo waandamanaji wamelaani vikali hatua ya kupiga marufuku vazi la kuogelea linalovaliwa na wanawake wa Kiislamu 'burqini' katika pwani za Ufaransa. Washiriki katika maandamano hayo wamesema kuwa, ongezeko kubwa la Waislamu linaloshuhudiwa hivi sasa, limeenda sambamba na kuibuka kwa harakati za chuki dhidi ya Uislamu na kwamba hivi sasa wanawake wa Kiislamu wanatumiwa kisiasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu nchini Ufaransa, ambapo safari hii yamelengwa mavazi yao ya heshima.

Askari mjini London wakiwazuia wanaharakati kufika kwenye ubalozi wa Ufaransa

Kufuatia hali hiyo waandamanaji hao mbali na kulaani vitendo hivyo, wamesema kuwa hilo ni suala lisilokubalika. Maandamano kama hayo yameshuhudiwa pia mjini Berlin huko Ujerumani ambapo waandamanaji walipiga kambi mbele ya ubalozi wa Ufaransa na kuonyesha hasira zao kali dhidi ya hatua hizo za serikali ya Paris. Katika siku za hivi karibuni kumeenea picha kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha askari wa Ufaransa akimlazimisha mwanamke wa Kiislamu kuvua vazi lake la staha.