Viongozi wa dini tofauti wafanya mkutano kuwaunga mkono Waislamu Marekani
(last modified Tue, 30 Aug 2016 04:35:32 GMT )
Aug 30, 2016 04:35 UTC
  • Viongozi wa dini tofauti wafanya mkutano kuwaunga mkono Waislamu Marekani

Viongozi wa dini tofauti katika mji wa Concord katika jimbo la New Hampshire nchini Marekani, wamefanya mkutano kwa ajili ya kutangaza uungaji mkono wao kwa Waislamu wa nchi hiyo.

Mtandao wa habari wa Concord Monitor umeandika kuwa, mkutano huo uliopewa jina la 'Onyesha Ujirani wa Upendo' uliitishwa kwa ajili ya kuondoa chuki dhidi ya Waislamu na kuwaunga mkono wafuasi wa dini hiyo. 

Mwanamke wa Kiislamu Marekani

Chris Scholtz, mkuu wa baraza la dini katika mji wa Concord amesema kuwa, mkutano huo umefanyika kwa ajili ya kuwakutanisha pamoja wafuasi wa dini tofauti na kujadili ajenda za kuwaunga mkono Waislamu hususan baada ya mauaji ya hivi karibuni ya imamu wa jamaa wa msikiti mmoja mjini New York na msaidizi wake.

Waislamu nchini Marekani wakilaani chuki dhidi yao

Naye Charles Edward kutoka kanisa la Paul Episcopal mjini hapo Concord alihutubia mkutano huo kwa kusema, kamwe amani haiwezi kupatikana endapo watu wote hawatakuwa pamoja.

Waislamu nchini Marekani

Ni vyema kuashiria kuwa, mauaji kadhaa ambayo yamekuwa yakihusishwa na ugaidi nchini Marekani yamesababisha kuongezeka kwa wimbi la chuki dhidi ya Uislamu, yakiwemo mashambulizi dhidi ya misikiti na maeneo ya ibada ya Waislamu. Aidha kuuawa, kupigwa na kutukanwa Waislamu nchini Marekani ni moja ya vitendo vya chuki vilivyoshika kasi hivi karibuni nchini humo.