Jamii ya Waislamu Ujerumani yalaani kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i14899-jamii_ya_waislamu_ujerumani_yalaani_kuongezeka_chuki_dhidi_ya_uislamu
Jamii ya Waislamu nchini Ujerumani imelaani vikali mwenendo wa kuongezeka chuki dhidi ya dini ya Kiislamu katika nchi hiyo ya bara Ulaya.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Sep 08, 2016 09:51 UTC
  • Jamii ya Waislamu Ujerumani yalaani kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu

Jamii ya Waislamu nchini Ujerumani imelaani vikali mwenendo wa kuongezeka chuki dhidi ya dini ya Kiislamu katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

Waislamu wa Ujerumani mbali na kulaani wimbi la chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu wameelezea wasiwasi walionao kutokana na kuweko ubaguzi nchini Ujerumani.

Ayman Mazyek, Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani (ZMD) ametangaza kuwa, vitendo vya hujuma na mashambulio dhidi ya misikiti vilionekana kushadidi nchini Ujerumani baina ya mwaka 2014 na 2015 huku vitendo vya hujuma dhidi ya wahajiri nchini humo vikionekana kuongezeka.

Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani (ZMD) amesisitiza kuwa, vitendo vya kurushiwa maneno na wakati mwingine hata kupigwa Waislamu navyo vinaonekana kuongezeka  mno katika barabara za ujerumani. 

Uislamu ni dini ya amani

Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani (ZMD) ameongeza kuwa, jamii ya Waislamu nchini humo wana wasiwasi mkubwa na sera za Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kuhusiana na wahajiri.

Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa, wanawake Waislamu wenye kuvaa hijabu pamoja na mashekhe wenye kuva kofia na vilemba wamekuwa wakisumbuliwa na kunyanyaswa na makundi  yenye kufurutu ada. 

Aidha inaripotiwa kwamba, takriban kila wiki msikiti mmoja hushambuliwa ima kwa mawe au kwa mabomu ya petroli na vijana wa makundi yanayoeneza chuki dhidi ya Uislamu nchini Ujerumani.

Hata hivyo licha ya propaganda na chuki dhidi ya Uislamu zinazoenezwa na makundi ya kuchupa mipaka, dini ya Kiislamu inaelezwa kuwa ndiyo dini inayokuwa kwa kasi kubwa barani Ulaya.