Uturuki yaitaka rasmi Marekani kumtia mbaroni Fethullah Gülen na kumkabidhi kwake
Serikali ya Uturuki imeitaka rasmi Marekani kumtia mbaroni Fethullah Gülen na kumkabidhi kwake.
Wizara ya Sheria ya Uturuki imetoa rasmi ombi hilo kwa Marekani hii leo, na kuongeza kuwa hatua hiyo inatokana na shakhasia huyo kuhusika katika kupanga na kuongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli hapo tarehe 15 Julai mwaka huu. Hii ni katika hali ambayo kabla ya hapo serikali ya Ankara ilikuwa imezifungia shule, taasisi na mashirika yanayomuunga mkono kifedha Fethullah Gülen, huku kwa mara kadhaa ikiitaka Washington kumrejesha Uturuki mwanasiasa huyo.
Hata hivyo na pamoja na hayo serikali ya Marekani bado haijatekeleza takwa hilo la Uturuki. Inafaa kukumbusha kuwa, Fethullah Gülen ambaye amewahi kuwa imamu, na hatibu mashuhuri nchini Uturuki, ni kiongozi wa harakati ya 'Khidmah' huku akiwa anaishi jimbo la Pennsylvania nchini Marekani. Gülen amekadhibisha tuhuma za Uturuki dhidi yake za kuhusika katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli hivi karibuni nchini humo.