Russia: Kauli ya Marekani ni dhihirisho kuwa inaunga mkono ugaidi
Serikali ya Moscow imesema matamshi ya hivi karibuni ya Marekani kuwa magaidi wa Daesh wanaofanya mashambulizi dhidi ya Syria yumkini wakaanza kuishambulia miji ya Russia ni ithibati tosha kuwa Washington inaunga mkono ugaidi.
Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amekosoa vikali matamshi yaliyotolewa jana Jumatano na John Kirby, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani kuwa magaidi wanaoendeleza harakati zao nchini Syria huenda wakaanzisha mashambulizi dhidi ya miji ya Russia karibuni hivi.
Amesema kuwa kauli hiyo ni sawa na kuwaalika magaidi wa ISIS/Daesh kuishambulia Russia na kwamba kwa mara nyingine tena Washington imeweka bayana kuwa ni muungaji mkono wa harakati za kigaidi duniani.
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia ameogeza kuwa, pendekezo la Marekani la usitishaji vita kwa muda wa siku 7 nchini Syria halikubaliki na kusisitiza kuwa Moscow inapendekeza muda huo wa usitishaji vita kwa msingi wa ubinaadamu uwe wa masaa 48 mjini Aleppo.
Russia imekuwa ikiliunga mkono jeshi la Syria katika juhudi zake za kuukomboa mji wa Aleppo kutoka mikononi mwa matakfiri wa Daesh.