Maadui wazidi kuonesha chuki zao dhidi ya Waislamu nchini Ujerumani
Magenge yenye misimamo ya kuchupa mipaka ya nchini Ujerumani yameendelea kuonesha chuki zao dhidi ya Waislamu kwa kutupa kichwa cha nguruwe nje ya msikiti wa mji wa Potsdam, makao makuu ya mkoa wa Brandenburg, nchini Ujerumani.
Jarida la Focus la nchini Ujerumani limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, siku ya Jumamosi usiku, kundi moja la watu wenye misimamo ya kuchupa mipaka lilitupa kichwa cha nguruwe nje ya msikiti wa mji wa Potsdam ikiwa ni kuvunjia heshima waziwazi matukufu ya Kiislamu.
Msikiti huo ni sehemu pekee ya Waislamu kwa ajili ya kufanyia ibada katika mji huo. Idadi ya Waislamu imekuwa ikiongezeka sana kwenye msikiti huo kiasi kwamba hivi sasa nafasi yake imekuwa ndogo na haitoshi kwa ajili ya Waislamu wanaomiminika kufanya ibada ndani ya msikiti huo.

Hivi karibuni meya wa mji huo aliwaahidi Waislamu kuwa atawasaidia kuwapata eneo kubwa zaidi la kujenga msikiti mkubwa kwa ajili ya kufanyia ibada.
Imam wa msikiti huo ameyalalamikia vikali makundi ya maadui hao wa Uislamu na kusema kuwa, baadhi ya wanasiasa nchini Ujerumani wanachochea chuki dhidi ya Waislamu.
Amesema, hii si mara ya kwanza maadui hao wa Uislamu kuonesha chuki zao dhidi ya Waislamu. Wiki iliyopita pia, watu wasiojulikana waliandika maandishi ya chuki na ya kibaguzi na kuyabandika kwenye kuta za msikiti huo. Miongoni mwa maandishi hayo yalisema: "Sisi ni Wajerumani, hatutaki Uislamu" na "Misikiti yote lazima ifungwe nchini Ujerumaini" pamoja na "Hijabu ni marufuku."