Ushindi wa Trump wawafanya raia wa Marekani kuandamana kuwaunga mkono Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i19339-ushindi_wa_trump_wawafanya_raia_wa_marekani_kuandamana_kuwaunga_mkono_waislamu
Raia wa jimbo la Texas nchini Marekani wamefanya maandamano kutangaza uungaji wao mkono kwa jamii ya Waislamu wa nchi hiyo kufuatia ushindi wa Donald Trump, rais mteule.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 12, 2016 11:01 UTC
  • Ushindi wa Trump wawafanya raia wa Marekani kuandamana kuwaunga mkono Waislamu

Raia wa jimbo la Texas nchini Marekani wamefanya maandamano kutangaza uungaji wao mkono kwa jamii ya Waislamu wa nchi hiyo kufuatia ushindi wa Donald Trump, rais mteule.

Mtandao wa habari wa TWC News umeripoti kuwa, wakazi wasio Waislamu wa mji wa Austin jimboni hapo waliandamana Ijumaa ya jana mbele ya msikiti wa eneo la Nueces kuwaunga mkono Waislamu na kuonyesha radiamali yao juu ya ushindi wa Trump katika uchaguzi wa rais wa hivi karibuni nchini humo.

Maandamano ya Wamarekani wanaompinga Trump

Katika maandamano hayo, Wamarekani hao wasio Waislamu walibeba mabango na maberamu yaliyokuwa na jumbe tofauti baadhi zikisema, 'urafiki utashinda chuki' na 'sisi sote ni watu wa taifa moja.' Arian Hom, mmoja wa washiriki wa maandamano hayo alinukuliwa akisema kuwa, Wamarekani wote wanatakiwa kuwaunga mkono Waislamu ili kuwafanya nao waweze kuhisi amani na usalama.

Sehemu ya mbinyo dhidi ya Waislamu wa Marekani

Naye Mohammed Omar Ismail, imamu wa jamaa wa msikiti wa mji wa Austin amesema kuwa, uungaji mkono wa raia hao wasio Waislamu kwa jamii ya Waislamu na katika kipindi hiki ambacho kinatawala siasa za kibaguzi nchini, ni jambo muhimu sana. Hayo yanajiri kufuatia ushindi wa Donald Trump, aliyetangazwa mshindi tarehe nane ya mwezi huu, ambaye katika kipindi cha kampeni zake kwa mara kadhaa alitangaza wazi kuwa, endapo atashinda uchaguzi, atawazuia Waislamu kuingia nchini humo.

Waislamu nchini Marekani

 

Inafaa kuashiria kuwa, tangu mfanyabiashara huyo mashuhuri atangazwe kuwa mshindi, vitendo vya ubaguzi nchini Marekani vimeongezeka. Aidha maandamano na machafuko ya kupinga ushindi wa Trump yameendelea kushuhudiwa katika maeneo mengi ya nchi hiyo huku karibu watu 20 wakiripotiwa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Waislamu Marekani wakionyesha hisia zao