Diplomasia ya Russia; kustawisha uhusiano na Iran
Katika kipindi hiki, Tehran imekuwa ikifikiwa na ugeni wa viongozi na maafisa wa nchi mbalimbali za Ulaya. Wakati László Kövér, Spika wa bunge la Hungary akiwa bado mjini Tehran kwa mazungumzo na mashauriano na maafisa wa Iran juu ya uhusiano wa mabunge ya nchi mbili Mwenyekiti wa Baraza la Shirikisho la Russia Valentina Ivanovna Matvienko, naye pia amewasili Tehran kwa safari rasmi ya kikazi.
Akiongoza ujumbe wa kibunge, Bi Valentina Matvienko aliwasili hapa nchini siku ya Jumapili kwa safari ya siku mbili ili kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran juu ya masuala ya pande mbili na ya kieneo.
Uhusiano wa Tehran na Moscow ni wa upeo wa kistratijia. Nchi hizi mbili zimeonyesha kivitendo kuwa zina sera endelevu na athirifu kuhusiana na matukio ya kieneo na kimataifa na wala hazipotezi fursa za ushirikiano. Kwa sababu hiyo viongozi wa nchi mbili wa ngazi tofauti wamekuwa wakikutana mara kwa mara na kufanya mazungumzo na mashauriano ya mtawalia. Kikao cha pande tatu cha marais wa Iran, Russia na Azerbaijan kilifanyika miezi michache iliyopita; na baada ya mazungumzo aliyofanya Rais Vladimir Putin wa Russia na viongozi wa Iran, hivi sasa maafisa wengine wa ngazi za juu wa Russia wamekuja mjini Tehran.
Iran na Russia zimekuwa na mazungumzo na ushirikiano wa karibu kwa kuzingatia maslahi na mitazamo ya pamoja katika uga wa masuala ya kieneo na kimataifa na vilevile kuhusiana na makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Ushirikiano huo hasa kuhusiana na mgogoro wa Syria una umuhimu wa kistratijia
Katika mazungumzo na Mwenyekiti wa Baraza la Shirikisho la Russia, Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) ameashiria mchango wenye taathira wa Russia katika matukio ya eneo ikiwemo kupambana na ugaidi na kueleza kwamba, kwa kusaidiana, Tehran na Moscow zinaweza kurejesha amani na usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia. Mbali na uhusiano wa kistratijia baina ya Iran na Russia, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya pia zimesisitiza mara kadhaa kuwa zina hamu ya kustawisha uhusiano na ushirikiano na Iran katika ngazi tofauti.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitakidi kuwa majimui ya nchi za Ulaya inaweza kutoa mchango athirifu zaidi katika masuala ya kieneo na kimataifa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif, aliashiria nukta hii ya msingi juu ya suala hilo katika mazungumzo aliyofanya na Spika wa Bunge la Hungary na kueleza kwamba katika zama hizi, siasa za ngoja ngoja haziwezi kutoa jibu kwa masuala ya ulimwengu. Matamshi hayo ya Zarif yanaashiria changamoto tunazoshuhudia leo hii katika eneo na duniani kwa jumla.
Kama katika miaka kadhaa nyuma nchi za eneo zingekuwa zimetekeleza sera zilizoratibiwa kuhusiana na mustakabali wa eneo hili, na laiti kama nchi hizo zisingetafuta visingizio vya kuhalalisha udhaifu wao wa kushindwa kutatua matatizo hasa katika uga wa usalama kwa kuyategemea madola ya nje ya eneo, leo hali ya eneo hili ingekuwa tofauti kabisa; na ugaidi usingeweza kujiepenyeza kwa kiwango kama kinachoshuhudiwa.
Hakuna shaka kuwa kushamiri na kuenea ugaidi na ugumu wa kupambana nao vimetokana na uungaji mkono wa baadhi ya nchi ikiwemo Marekani kwa uovu huo ambao Washington inautumia kama wenzo wa kudhamini maslahi yake katika eneo hili la Magharibi mwa Asia.
Katika hali kama hii kuimarishwa uhusiano na kuongezwa ushirikiano katika suala hilo kunaweza kusaidia kuzivuka changamoto na kukabiliana na vitisho vya pamoja vinavyoyakabili mataifa ikiwemo ugaidi, misimamo ya kufurutu mpaka na magendo ya mihadarati. Na hili ni suala lililotiliwa mkazo pia katika kikao cha siku ya Jumapili cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kilichofanyika mjini Brussels.
Katika mazungumzo aliyofanya hapo kabla na viongozi wa Iran, Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya aligusia pia nukta hiyo na kueleza kwamba Umoja wa Ulaya umeazimia kwa dhati kustawisha ushirikiano wake na Iran kwa ajili ya kudhamini maslahi ya pamoja ya pande mbili.../