Amnesty yaikosoa Kenya kwa kuwafukuza wakimbizi kutoka Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i19528-amnesty_yaikosoa_kenya_kwa_kuwafukuza_wakimbizi_kutoka_somalia
Shirika la haki za binadmau la Amnesty International limeikosoa serikali ya Kenya kwa kuwalazimisha wakimbizi kutoka Somalia kurejea katika nchi yao inayokumbwa na vita na hivyo kuhatarisha maisha yao.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 15, 2016 14:15 UTC
  • Amnesty yaikosoa Kenya kwa kuwafukuza wakimbizi kutoka Somalia

Shirika la haki za binadmau la Amnesty International limeikosoa serikali ya Kenya kwa kuwalazimisha wakimbizi kutoka Somalia kurejea katika nchi yao inayokumbwa na vita na hivyo kuhatarisha maisha yao.

Katika taarifa siku ya Jumanne, Amnesty imesema idadi kubwa ya wakimbizi wanaorejea nchini kwao wanakabiliwa na hatari ya kuuawa au kuingizwa kwa nguvu katika kundi la kigaidi la al Shabab linalofungamana na Al Qaeda.

Mwezi Mei Kenya ilitangaza nia yake ya kufunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab, ambayo ni kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani. Kenya ilikuwa imepanga kuifunga kambi hiyo yenye wakimbizi 280,000 ifikapo mwezi Desemba.

Serikali ya Kenya inasema baadhi ya wakimbizi katika kambi ya Dadaab, iliyo karibu na mpaka wa Kenya na Somalia, huwa wanatumiwa na magaidi wa al Shabab kutekeleza hujuma za kigaidi nchini humo.

Kambi ya Wakimbizi ya Dadaab

Amnesty inasema kuwafurusha wakimbizi bila hiari yao ni kinyume cha hakikisho la Kenya kwa jamii ya kimataifa kuwa itahakikisha wakimbizi wanarejeswa makwao pale wanapotaka na zoezi kama hilo lifanyike kwa usalama na heshima.

Msemaji wa serikali ya Kenya Mwenda Njoja, jana Jumatatu alisema serikali haitaweza kufunga kambi hiyo mwezi Desemba kama ilivyokuwa imepangwa. Ameongeza kuwa kati ya Mei na Oktoba mwaka huu, zaidi ya wakimbizi 30,000 wamerejea Somalia kwa hiari yao.