Iran na Russia kuendeleza ushirikiano wa vita dhidi ya ugaidi
Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia wamesisitiza kuhusu kuendeleza ushirikiano katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Rais Hassan Rouhani wa Iran na mwenzake wa Russia Vladimir Putin wamezungumza kwa njia ya simu Jumatatu usiku ambapo waliashiria mitazamo ya pamoja na ushirikiano wa nchi mbili katika vita dhidi ya ugaidi ahsa nchini Syria na kusema ushirikiano huo na taathira za kihistoria. Aidha wamesema njia pekee ya kutatua mgogoro wa Syria ni kupitia mazungumzo ya kisiasa na kuheshimiwa haki za taifa la Syria katika kuainisha mustakabli wa nchi hiyo.
Rais Rouhani amebainisha furaha yake kutokana na mwenedo chanya wa ushirikiano wa Iran na Russia na kusema kikao cha tume ya pamoja na ushirikiano wa nchi mbili kitafanyika hivi karibuni mjini Tehran. Ameelezea matumaini yake kuwa kikao hicho kitatoa msukumo zaidi kwa uhusiano wa nchi mbili ikiwa ni pamoja na kurahisisha ushirikiano wa kibenki na kuondolewa visa.
Kwa upande wake Rais Vladmir Putin wa Russia ameashiria ushirikiano wa Iran na nchi yake katika masuala ya eneo na kusema: "Tehran na Moscow ni washirika katika utatuzi wa masuala ya eneo na mitazamo ya pamoja na ushurikiano wa pande mbili hasa kuhusu Syria utaendelea hadi Wasyria wakombolewe kutoka mikononi mwa magaidi."
Rais wa Russia amesema nchi yake itafadhili miradi ya pamoja ya nchi mbili ikiwa ni pamoja na mradi wa kituo cha nyuklia cha Bushehr, kuweka umeme katika njia ya reli ya Incheburun kaskazini mwa Iran hadi Garmsar mashariki mwa Tehran. Aidha marais hao wawili wamejadili matukio ya hivi karibuni katika soko la mafuta la Iran na udharura wa ushurikiano zaidi wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani