Dec 13, 2016 08:21 UTC
  • Wananchi wa Azerbaijan waandamana dhidi ya safari ya Netanyahu

Wananchi wa Azerbaijan wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo Baku, kulaani safari ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu ambaye anaanza ziara isiyo ya kawaida katika nchi mbili za Kiislamu za Asia ya Kati.

Wafuasi wa Chama cha Kiislamu cha Azerbaijan wamekusanyika nje ya Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo mjini Baku, wakilalamikia safari ya Netanyahu nchini humo.

Wanafunzi wa vyuo vikuu jana Jumatatu nchini walifanya maandamano katika mkoa wa Ardabil, ulioko katika mpaka wa nchi hiyo na Iran kulaani safari hiyo ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel. Wanachuo hao walisikika wakipiga nara za kulaani safari hiyo ya Netanyahu ambaye ametenda jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina.

Ramani inayoonyesha Azerbaijan na nchi jirani zake

Netanyahu anatazamiwa kuitembelea Azerbaijan kwa muda wa masaa saba pekee na kisha kuelekea katika nchi ya Kazakhstan.

Azerbaijan inatajwa kuwa moja wa nchi zenye uhusiano mzuri wa kibiashara na utawala khabithi wa Israel, haswa kwa kutilia maanani kuwa asilimia 40 ya mafuta ya Tel Aviv yananunuliwa kutoka serikali ya Baku. Kadhalika Azerbaijan na Israel zinashirikiana katika masuala ya kijeshi.

Ziara ya Netanyahu katika nchi mbili hizo za za Kiislamu za Asia ya Kati inajiri katika hali ambayo, utawala haramu wa Israel unaendelea kuzikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina uliozighusubu, mbali na kuwaua, kuwafunga jela na kuwakandamiza wananchi madhulumu wa taifa la Palaestina kila leo.

 

Tags