Waandishi karibu 100 wa habari wameuawa mwaka huu wa 2016
Federesheni ya Kimataifa ya Waandishi Habari (IFJ) imetangaza kuwa, waandishi habari 93 wameuawa kwa makusudi au katika machafuko yaliyotokea kwenye maeneo mbalimbali ya dunia katika mwaka huu unaomalizika leo wa 2016.
IFJ imesema kuwa, waandishi hao wa habari wameuawa katika nchi za Afrika, Asia, Pasific, America na Ulaya.
Federesheni ya Kimataifa ya Waandishi Habari imesema matukio mabaya zaidi kwa waandishi habari katika mwaka huu unaomalizika leo ni vifo vya maripota 20 wa Brazil baada ya ndege waliyokuwamo kuanguka katika mji wa Medellin nchini Colombia na vifo vya maripota 9 wa Russia wakati ndege iliyokuwa na nambari ya usajili Tu-154 ilipoanguka katika Bahari Nyeusi, mwezi huu wa Disemba.
Mwaka uliopita wa 2015 waandishi habari 112 waliuawa kote duniani katika matukio mbalimbali.
Federesheni ya Kimataifa ya Waandishi Habari ambayo iliasisiwa mwaka 1926, ndiyo jumuiya kubwa zaidi ya waandishi habari duniani. Jumuiya hiyo ina wanachama laki sita katika nchi 140 na lengo lake kuu ni kuimarisha na kuboresha haki na uhuru wa waandishi wa habari.