Kadhaa wauawa katika mapigano ya kikabila Sudan Kusini
(last modified Fri, 09 Jun 2023 01:24:49 GMT )
Jun 09, 2023 01:24 UTC
  • Kadhaa wauawa katika mapigano ya kikabila Sudan Kusini

Watu wasiopungua 13 wameuawa katika mapigano mapya ya kikabila katika nchi ya Sudan Kusini.

Duru za habari ziliripoti habari hiyo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, mbali na kuuawa raia 13, wengine wasiopungua 21 wamejeruhiwa katika mapigano hayo karibu na eneo linalomilikiwa na Umoja wa Mataifa.

Yoannes Kimo, Naibu Mwenyekiti wa asasi inayowakilisha wakimbizi wa ndani katika eneo hilo ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, mapigano hayo yaliibuka mapema jana katika eneo la Malakal, baina ya jamii za Shilluk na Nuer.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, mapigano hayo yalianza baada ya mtu mmoja kuchomwa kisu. Imetoa mwito kwa pande hasimu kuwa watulivu, huku ikiongeza idadi ya askari polisi na wanajeshi katika eneo hilo.

Kambi ya wakimbizi wa ndani eneo la Malakal

Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika yamepelekea watu zaidi ya 400,000 kuuawa, mbali na mamlioni kufurushwa kwenye makazi yao na kuwa wakimbizi katika kipindi cha miaka 8 iliyopita.

Rais Salva Kiir Mayardit alikiri katika hotuba yake ya karibuni kwamba, machafuko ya kikabila na kijamii yanatishia kurudisha nyuma mafanikio ya amani yaliyopatikana katika utekelezaji wa mkataba wa amani uliohuishwa wa 2018.