WHO yawataka walimwengu wazidishe mapambano dhidi ya sigara
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa mapambano dhidi ya sigara yanaweza kuokoa mabilioni ya fedha mbali na kuokoa maisha ya mamilioni ya wanadamu.
Ripoti iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) imeonesha kuwa, sera za kupambana na sigara na tumbaku ikiwa ni pamoja na kuweka ushuru na kodi kwa bidhaa hizo na kuzidisha bei zake vinaweza kudhamini pato kubwa kwa ajili ya sekta ya afya na maendeleo.
Oleg Chestnov ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa WHO amesema kuwa, hatua kama hizo zinaweza kupunguza sana kiwango cha utumiaji wa tumbaku na hivyo kuwalinda afya ya mamilioni ya watu duniani mbele ya wauaji wakubwa zaidi duniani yaani saratani na maradhi ya moyo.
Ripoti ya WHO imeongeza kuwa, kupandishwa bei ya bidhaa zinazotokana na tumbaku kunaweza kunyanyua juu kiwango cha afya ya walimwengu na kuokoa mabilioni ya dola za uchumi wa duniani.
Ripoti hiyo imeashiria uchunguzi uliofanyika mwaka jana na kusema kuwa: Iwapo nchi zote zitazidisha senti 80 tu kwa kila sigara moja mapato ya ushuru wa sigara duniani yanaweza kuongezeka kwa asilimia 47 yaani dola bilioni 140.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Shirika la Afya Duniani, karibu watu milioni sita hufariki dunia kila mwaka kutokana na utumiaji wa tumbaku na sigara.