Askari wastaafu wamtahadharisha Trump kuhusu mateso na unyanyasaji
Maafisa waliostaafu wa jeshi la Marekani wamemtaka rais mteule wa nchi hiyo azuie kurejeshwa sheria ya kuwatesa wadhaniwa wa mashambulizi ya kigaidi.
Maafisa 176 waliostaafu wa jeshi la Marekani wakiwemo majenerali 33 wamemwandikia barua Donald Trump wakimtahadharisha kuhusu utekelezaji wa aina mbalimbali za mbinu za kuwatesa watu wanaodhaniwa kuwa na uhusiano na vitendo vya kigaidi.
Wanajeshi hao wastaafu wameeleza wasiwasi wao kuhusu taarifa zilizotolewa na Donald Trump katika kampeni zake za uchaguzi wa rais kuhusu utumiaji wa mateso kwa ajili ya kuwasaili wadhaniwa katika korokoro za Marekani.
Miongoni mwa wanajeshi wastaafu waliotia saini barua hiyo ni Jenerali Stanley A. McChrystal na Jenerali John R. Allen, ambao wote walikuwa makamanda wa jeshi la Marekani huko Afghanistan.
Katika kampeni zake za uchaguzi wa rais, rais mteule wa Marekani Donald Trump alisisitiza kwamba atatumia mbinu kali zaidi za mateso na manyanyaso wakati wa kuwasaili washukiwa wa ugaidi.