UNESCO yatahadharisha kuhusu ukatili unaofanywa dhidi ya wanafunzi mashuleni
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limetangaza kuwa, mamilioni ya wasichana na wavulana hukumbana na unyanyasaji na uonevu wanapokuwa mashuleni katika maeneo mbalimbali ya dunia.
Ripoti iliyotolewa leo na UNESCO ikishirikiana na Taasisi ya Kuzuia Unyanyasaji Mashuleni imesema kuwa, ukatili mashuleni unatokana na uhusiano usio sawa nguvu na madaraka, vigezo vinavyohusiana na masuala ya jinsia, umaskini na masuala mengine kama utambulisho wa kitaifa.
Katibu Mkuu wa Unesco Irina Bokova amesema unyanyasaji na uonevu mashuleni ni ukiukaji mkubwa wa haki ya elimu na kwamba ripoti mpya ya shirika hilo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kwamba shule na vituo vingine vya elimu viko salama kwa watu wote.

Bokova ametahadharisha kuwa uonevu na unyanyasaji unaofanyika mashuleni ukiwemo unyanyasaji wa kimwili, kinafsi na kingono una taathira mbaya na kubwa kwa uwezo wa kusoma wa wanafunzi na uzima wa kimwili na kiroho.

Ripoti ya UNESCO pia imesema watoto na vijana waliokumbana na unyanyasaji wanakabiliwa na hatari ya msongo wa mawazo, hali ya kutojiamini, kujiona duni, kujitenga na mawazo ya kujiua.