Saudi Arabia yainyima Israel kibali cha kuhudhuria mkutano wa UNESCO
Shirika la habari la Sputnik la Russia limetangaza kuwa, Saudi Arabia imekataa kuwaruhusu wawakilishi wa utawala wa Kizayuni wa Isarel kuhudhuria mikutano ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambayo imepangwa kufanyika mjini Riyadh mwezi Septemba mwaka huu.
Ripoti hiyo imesema kuwa, Saudi Arabia bado haijatia saini hati ambayo itawaruhusu wawakilishi wa utawala wa Kizayuni kuhudhuria mikutano ya UNESCO mjini Riyadh.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanadiplomasia wa nchi za Magharibi na maafisa waandamizi wa utawala wa Kizayuni wamesema kuwa, Saudi Arabia haijaashiria utawala wa Kizayuni kuhusu kutosaini hati hiyo, lakini wameeleza wazi kuwa utawala wa Israel ndio tatizo kuu.
Ripoti zinasema, Saudi Arabia inaendelea kuwa na tahadhari kuhusu hatua zozote zinazofungua njia ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel.
Iwapo Saudi Arabia itakubali kuwepo wawakilishi wa Israel mjini Riyadh kushiriki katika vikao vya Kamati ya Turathi za Dunia, hii itakuwa mara ya kwanza kwa viongozi wa Kizayuni kuruhusiwa rasmi na kuingia Saudi Arabia waziwazi na bila ya kujificha.
Utawala haramu wa Israel unalaumiwa na mashirika na taaisi za kimataifa za kutetea haki za binadamu kwa kuendeleza mauaji dhidi ya raia hasa watoto wadogo wa Palestina.
Hapo awali, mkutano huo wa UNESCO ulipangwa kufanyika nchini Russia mwaka jana, lakini kutokana na tishio la baadhi ya nchi wanachama la kususia tukio hili, Saudi Arabia imepewa jukumu la kuwa mwenyeji wa mkutano huo.