Indhari ya UN kuhusu kuongezeka ukiukaji wa haki za binadamu duniani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu kuongezeka vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu duniani.
Antonio Guterres ametahadharisha kuhusu kuongezeka vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu na kulitaka Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo kufanya juhudi za kufuatilia na kukabiliana na tatizo hilo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika marasimu ya ufunguzi wa kikao cha kwanza cha kila mwaka cha Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo kuwa, kupuuzwa haki za binadamu ni maradhi ambayo yanaenea katika pande mbalimbali; na kwa msingi huo baraza hilo la Umoja wa Mataifa linapasa kuwa sehemu ya tiba ya maradhi hayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amelitaka Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo kuwa na nafasi kuu katika kuzuia ukiuaji wa haki za binadamu na kutoa tahadhari kwa migogoro inayoweza kutokea. Guterres ameongeza kuwa kamati za uchunguzi na makundi ya kutafuta ukweli duniani kote yanafanya kazi ya kuchunguza tuhuma za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu duniani. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo huo ametaka yawepo mashirikano mapana kati ya Baraza la Haki za Binadamu la UN na taasisa za kiraia ili kuzuia kutokea visa hivyo.