UN: Mazungumzo juu ya Syria huko Geneva, yametoa ajenda iliyo wazi
(last modified Sat, 04 Mar 2017 07:26:13 GMT )
Mar 04, 2017 07:26 UTC
  • UN: Mazungumzo juu ya Syria huko Geneva, yametoa ajenda iliyo wazi

Umoja wa Mataifa umepongeza duru ya hivi punde ya mazungumzo ya amani ya Syria iliyomalizika jana Ijumaa mjini Geneva nchini Uswisi.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura ameyataja mazungumzo hayo ya siku tisa kama ya kweli, huru na halisi na ambayo yameainisha ajenda iliyo wazi kwa ajili ya mustakabali wa nchi hiyo ya Kiarabu.

De Mistura amefafanua kuwa, duru ijayo ya mazungumzo hayo itajikita zaidi kuhusu stratejia za kupambana na ugaidi na usitishaji vita nchi nzima, kati ya wawakilishi wa serikali na makundi ya upinzani baadaye mwezi huu.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria amesema katika siku chache zijazo, atasafiri kwenda mjini New York kumtaarifu Antonio Guterres,

Bashar al-Jaafari, Balozi wa Syria UN

Katibu Mkuu wa umoja huo kuhusu mazungumzo hayo ya Geneva. Afisa huyo wa UN amesema mazungumzo ya Geneva na Astana ni juhudi zinazokamilishana za kukwamua mgogoro wa miaka 6 Syria.

Nassir al-Hariri, kiongozi wa Kundi kuu la upinzani linalojiita Kamati Kuu ya Mazungumzo amesema, kwa mara ya kwanza wamefanya mazungumzo na De Mistura kuhusu mpito wa kisiasa na maudhui zinazohusiana na suala hilo.

Amesema duru ya mazungumzo ya "Geneva 4" iliyokamilika imekuwa na mwelekeo chanya zaidi na imejadili kwa mapana kuhusu kipindi cha mpito wa kisiasa.