Russia yamuita Balozi wa Israel kuhusu shambulio dhidi ya Syria
Russia imemuita Balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mjini Moscow ajieleza kuhusu hatua ya jeshi la utawala huo kuhujumu anga ya Syria sambamba na kutekeleza mashambulizi kadhaa katika ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imemweka kwenye kiti moto Gary Koren, Balozi wa Israel mjini Moscow juu ya mashambulizi ya jeshi la anga la utawala huo haramu dhidi ya Syria na vilevile kuhujumu anga ya nchi hiyo.
Balozi huyo ametakiwa kutoa maelezo hayo siku moja baada ya kuwasilisha vyeti vyake kwa Rais Vladimir Putin wa Russia mjini Moscow.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la umoja huo kulaani chokochoko hizo za Israel.
Hii ni katika hali ambayo, Komandi Kuu ya Jeshi la Syria imetangaza kuwa kikosi cha anga cha jeshi la nchi hiyo kimetungua ndege ya kivita ya utawala haramu wa Israel wakati ilipokuwa ikielekea mji wa Palmyra, magharibi mwa mji wa Homs kuwasaidia magaidi walioshindwa wa Daesh.
Serikali ya Damascus imesema kuwa, baada ya magaidi wa genge la Daesh (ISIS) kushindwa na jeshi la Syria, hivi sasa utawala wa Kizayuni unafanya njama kila uchao kwa ajili ya kuwapa moyo magaidi hao katika vita vyao dhidi ya serikali halali ya Rais Bashar al-Assad.