Umoja wa Mataifa wawashutumu wanaoeneza uongo kuhusu Uislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27020-umoja_wa_mataifa_wawashutumu_wanaoeneza_uongo_kuhusu_uislamu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewashutumu watu wanaoeneza propaganda chafu dhidi ya Uislamu ambao wanajaribu kuihusisha dini hiyo na vitendo vya kigaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 29, 2017 09:48 UTC
  • Umoja wa Mataifa wawashutumu wanaoeneza uongo kuhusu Uislamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewashutumu watu wanaoeneza propaganda chafu dhidi ya Uislamu ambao wanajaribu kuihusisha dini hiyo na vitendo vya kigaidi.

Shirika la habari la IRNA limenukuu António Guterres akisema hayo leo katika kikao cha ufunguzi wa mkutano wa 28 wa viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Arab League nchini Jordan na kuongeza kuwa, kuna baadhi ya viongozi wa nchi wanafanya njama za kuuhusisha Uislamu na vitendo vya kigaidi.

Vile vile ameelezea kusikitishwa kwake na hatua ya baadhi ya nchi zilizoendelea ya kufunga mipaka yao na kutoruhusu wakimbizi kuingia katika nchi hizo na kusema kuwa, huko ni kwenda kinyume na makubaliano ya kimataifa.

Wahanga wakuu wa jinai za magenge ya kigaidi ni Waislamu, lakini pamoja na hayo maadui wa Uislamu wanaihusisha dini hiyo tukufu ya Mwenyezi Mungu na jinai za magenge hayo ya kigaidi. 

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aidha amesema, umoja huo uko tayari kushirikiana na ulimwengu wa Kiarabu katika jitihada za kuleta amani ya kudumu duniani. Amesema, wakati umefika wa kutatuliwa kikamilifu mgogoro wa Syria.

António Guterres ameelezea matumaini yake kuwa, mazungumzo ya Geneva yatasaidia kupatikana njia za kutatua mgogoro wa Syria na kwamba suala la kusimamisha mapigano kwa ajili ya kufikia utatuzi wa kudumu wa mgogoro wa nchi hiyo, ni jambo la dharura.

Aidha amesema, Umoja wa Mataifa unalaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kusisitiza kuwa, hakuna njia yoyote inayoweza kuzuia machafuko huko Palestina isipokuwa kuundwa nchi huru ya Palestina.